Jeshi la Magereza limefanikiwa kumkatamata Ramadhan Nombo mkazi wa
Mabibo jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kutaka kuingiza simu tano
kinyume cha sheria katika gereza la Keko wilayani Temeke.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Augustine Mboje jana alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni katika gereza hilo.
Alisema Nombo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kuanzia 30 na
kuendelea alidakwa wakati akifanyiwa upekuzi katika eneo maalumu la
ukaguzi wa wageni mbalimbali wakiwamo wanaowatembelea ndugu na marafiki
walioko mahabusu kwenye gereza hilo.
“Huyu (Nombo) alikuwa katika foleni ya mstari wa mwisho ya watu
wanaokwenda kuwaaona ndugu zao walioko ndani ya gereza hili. Nadhani
hakujua kama sisi kama magereza tuna vifaa vya kisasa vya ukaguzi.
“Ilipofika zamu yake askari wetu walimfanyia ukaguzi na kabla haujaisha
kifaa hiki maalumu kiliita alamu kuashiria kuna kitu tofauti,” alisema
Mboje.
Alisema alibainika kuwa na simu hizo alizozifunga kitaalaamu na kuficha
katika mapande ya nyama yaliyopikwa kwa ustadi wa juu na kuchanganywa na
viazi aina ya mbatata.
Mkuu huyo wa magereza, alisema tukio hilo siyo la kwanza katika gereza
hilo kwani linatokea katika magereza mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam
likiwamo la Segerea.
“Wengine wanatumia hadi mbinu ya kuficha simu hizi katika ugali na
mikate lakini tunafanikiwa kuwakamata kutokana na uimara wa vifaa na
askari wetu,”alisema Mboje
Hakuna maoni: