Mbunge
wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amefunguka na kuwataka wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi na wale wa upinzani kuungana pamoja katika kupigania
rasilimali za nchi katika vita ambayo imeanzishwa na Rais Magufuli.
Nape
Nnauye amesema hayo bungeni na kuwataka watu wa CCM wasipuuze mawazo
ambayo yanatolewa na watu wa upinzani na kusema wanapaswa kuyafanyia
kazi ili mwisho wa siku nchi iweze kufaidika na rasilimali hizo na
kuwafanya kuwa pamoja katika jambo hilo na si kunyoosheana vidole.
"Katika
hili tunaweza kugawanyika katika mitazamo wapo wale wanaounga mkono
asilimia mia moja, wapo wale wanaopinga kwa namna wanavyowaza wao sasa
kelele zisiturudishe nyuma lazima tusonge mbele sababu vita hii ni
takatifu.
"Lakini
tusipuuze kwani katika kelele nyingi kunaweza kuwa na ushauri mzuri
ndani yake, isifike mahali tukapuuza kabisa hii vita ni ya kwetu wote,
nchii hii ikifaidika katika jambo hili ni faida kwetu wote bila kujali
itikadi zetu za vyama, sasa tusitoboane macho, tusitupiane vijembe
visivyokuwa na maana ni wakati wa kuileta nchi yetu pamoja twende pamoja
vita hii tushinde, kwa hiyo wapinzani na CCM na watu wengine wote bila
kujali itikadi zetu nadhani ni vizuri tukaungana katika hili"alisisitiza Nape Nnauye
Mbali
na hilo Nape Nnauye alisema kuwa anachokifanya Rais Magufuli sasa
anapita katika msingi ambao watangulizi wake waliuweka hivyo anadai
viongozi hao wastaafu walifanya kazi kubwa kulinda rasilimali za nchi
kwa uwezo wao, hivyo dhana ya kuona hawakuwa na jitihada za kulinda
rasimali hizo si sawa.
"Hizi
juhudi za kulinda rasilimali za nchi yetu hazijaanza awamu ya tano,
zimeanza toka awamu ya kwanza ya mwalimu Nyerere kuna mambo alifanya
kulinda rasilimali zetu hata kama kutakuwa na mapungufu, awamu ya pili
ya mzee Mwinyi yapo mambo aliyafanya, awamu ya tatu ya mzee Mkapa yapo
mambo aliyafanya, awamu ya nne ya Mhe. Kikwete yapo mambo ameyafanya
mazuri tu, kwa hiyo hakuna namna tutapuuza juhudi zilizofanywa na
watangulizi wa Mhe. Magufuli kwa sababu nao wana mchango hata kama leo
itaonekana kulikuwepo na mapungufu lakini kwa nafasi zao walitimiza
wajibu wao" alisema Nape Nnauye
Hakuna maoni: