Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine
Matiro(pichani) amepiga marufuku tabia ya wazazi kuwasafisha nyota
watoto wa kike kwa kuwaogesha dawa inayojulikana kwa jina la “Samba”
ili wapendwe na wanaume kwani ni kichocheo kikubwa cha mimba na ndoa za
utotoni matokeo yake wanafunzi wanakatisha masomo yao shuleni.
Matiro alipiga marufuku tabia hiyo ya
kuwapa dawa ya mapenzi watoto jana wakati wa maadhimisho ya tatu ya siku
ya maadhimisho ya Siku ya Chama Cha Wanawake na Wasichana( Young
Women's Christian Association- YWCA) duniani ambayo kwa kanda ya Ziwa
Victoria yaliyofanyika katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga na
kukutanisha wadau kutoka mikoa ya Mara,Mwanza na Shinyanga.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kidunia
ni "Kuunda Ulimwengu Unaojumuisha Wote" huku kauli mbiu ya maadhimisho
hayo kanda ya ziwa ikiwa ni "Kwa Pamoja Tuzuie Ndoa na Mimba za
Utotoni,Tutaleta Mabadiliko Kielimu".
Akizungumza katika maadhimisho
hayo,Matiro ambaye ni kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga alisema amepewa
taarifa kuwa wazazi wengi mkoani Shinyanga wana tabia ya kuwapeleka
watoto wa kike kwa waganga wa jadi kupewa “samba”(kupewa dawa ya
kusafisha nyota ili wawe na mvuto kwa wanaume.
“Nitakaa na kamati ya ulinzi na usalama
niagize wale waganga wote wanaosafisha nyota za watoto wa kike
tuwakamate kwa sababu hatuwezi kusema tunamtetea mtoto asipate mimba
wakati mtoto huyo anaenda kuogeshwa asafishe nyota,yupo darasa la
tano,kwani akili yake imeshabadilishwa tayari kwamba mimi natakiwa
nipendwe,natakiwa nifanyiwe hivi,je atasoma?”,alihoji Matiro.
Matiro alisema suala la ndoa na mimba za
utotoni ni janga kubwa katika kanda ya ziwa hususani mkoa wa Shinyanga
ambao unaongoza kitaifa kwa asilimia 59 ukifuatiwa na mkoa wa Tabora na
Mara hivyo ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuwalinda watoto.
“Naombeni mbadilike,leo wewe mzazi
unafurahia kumpeleka mtoto wako asafishwe nyota ili apendwe na
wanaume,akipata mimba akiwa shuleni unaanza kushangaa wakati wewe ndiyo
chanzo cha matatizo”,aliongeza Matiro.
Katika hatua nyingine aliwataka wazazi
kuwa karibu na watoto wao na kuwapa elimu juu ya uzazi wa mpango badala
ya kuwaonea aibu matokeo yake wanajiingiza katika vitendo viovu
vinavyosababisha wapate mimba na kuolewa wakiwa wadogo.
Aidha alivitaka vikundi vya akina mama
katika jamii kujenga tabia ta kukutana na mabinti katika mitaa na vijiji
na kuwapa elimu ya uzazi wa mpango ili kupunguza na hata kuondoa kabisa
tatizo la mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga.
Kwa upande wake Katibu wa YWCA mkoa wa
Shinyanga Maryciana Makundi,akisoma risala kwa mgeni rasmi ambaye ni
Josephine Matiro alisema watoto wengi wa kike wanalazimishwa kuolewa
kutokana na wazazi kuwa na tama ya mali,elimu duni,mfumo dume kutawala
familia akidai kuwa hata kama mama hataki,hana mamlaka ya kuzuia baba
asifanye atakavyo.
Makundi alisema pia watendaji katika kuwasaidia watoto kisheria huwageuka na kupkea rushwa kwa wahalifu kitendo ambacho kuwavunja moyo wahanga wa ukatili.
Aliongeza kuwa kesi nyingi za watoto waliobakwa zimekuwa zikiahirishwa kila mara licha ya kuwepo ushahidi ulio wazi dhidi ya watenda uovu na wakati mwingine kesi hazisikilizwi kabisa na zingine ushahidi hupotezwa,kukatiwa rufaa na baadhi kuzungushwa na baadhi ya wanasheria kwa maksudi yasiyokuwa ya wazi
Hakuna maoni: