MTOTO Prince lsaack (10) mwanafunzi wa darasa la 5,
mkazi wa Kata ya Kihonda, Maghorofani mkoani hapa, amefariki dunia
wakati akiogelea mtoni na wenzake.
Prince alifikwa na mauti Jumapili iliyopita saa 7 mchana wakati
akienda kanisani lakini kabla ya kufika huko waliamua kuogelea katika
Mto Ngerengere bila kujua hatari iliyokuwa mbele yake.
Akizungumza na Ijumaa kuhusiana na kifo hicho, mama mzazi wa marehemu, Sarah Mwanjaa alisema amehuzunishwa mno na tukio hilo.
Mama huyo aliongeza kuwa, amepata pigo kubwa sana kuondokewa na
Prince ambaye yeye na mwenzake ndiyo walikuwa faraja yake kufuatia
kufiwa na mumewe.
Akizungumzia tukio hilo alisema kwamba siku ya tukio
alimwambia marehemu ikifika saa 8 mchana ale kisha aende kwenye ibada ya
watoto katika kanisa wanalosali la Tanzania Assembulies of God
lililopo Mwembesongo.
“Kwa kuwa ibada ya wakubwa inafanyika saa 4 asubuhi nilimuaga,
nikaelekea kanisani na kusisitiza ikifika saa nane awahi kanisani,
nikaondoka bila kujua kama nilikuwa namuaga mwanangu,” alisema mama
huyo.
Aliongeza kuwa, ilipofika saa 8 mchana hakumuona mwanaye kanisani
akapata wasiwasi na kuamua kurudi nyumbani ambako alimkuta rafiki wa
marehemu aitwaye Steve akiwa ameshika nguo za mwanaye akamwambia
walikuwa wanaogelea lakini mwenzake alizama mtoni. “Baada ya kupewa
taarifa hiyo nilianza kulia ndipo walitokea majirani zangu nikawaambia
kilichotokea, wakaenda kutoa taarifa kwa afisa mtendaji, Godfrey Maumba
wakaanza kumtafuta bila mafanikio kwa muda wa siku tatu,” alisema mama
huyo.
Aliongeza kuwa baada ya kumtafuta usiku na mchana bila mafanikio,
siku ya nne alipatikana akiwa amekufa huku baadhi ya sehemu za mwili
wake zikiwa zimenyofolewa na mamba. Akizungumza na Ijumaa kuhusiana na
tukio hilo, afisa mtendaji wa kata hiyo, Maumba alikiri kutokea tukio
hilo na kusema wamepata pigo kubwa sana kumpoteza mtoto huyo mdogo.
Naye Diwana wa Kata hiyo, Lydia Mbihaji akizungumza na paparazi wetu
kuhusiana na tukio hilo alisema amesikitika sana na akatoa rai kwa
wazazi kuwa makini na watoto wao. Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro,
Leonard Paulo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Prince na gazeti
hili linaipa pole familia yake na kumuomba Mungu awape nguvu katika
kipindi hiki kigumu.
Hakuna maoni: