Vurugu kubwa zimetokea katika kijiji cha Buyango wilayani Muleba
mkoani Kagera baada ya wazazi kuikataa maiti ya mtoto wao kwa madai
amenyofolewa viungo vyake vya mwili hali iliyosababisha polisi kutumia
mabomu ya machozi kutawanya makundi yaliyofunga barabara na kubomoa
chumba cha kuhifadhia maiti kutafuta viungo hivyo.
Vurugu hizo zimetokea baada ya mama mmoja mkazi wa
Arusha aliyepeleka maiti ya mtumishi wake wa ndani na kuwakabidhi wazazi
wake kwa masharti ya kutoifunua hali iliyosababisha mtafaruku mkubwa
ambapo mama huyo amelazimika kwenda hospitali kukabidhi mwili huo ambapo
baadhi ya ndugu na jamaa walivamia chumba cha kuhifadhi maiti na kubomoa
mlango kisha waka angalia mwili ambao wameukuta ukiwa na majeraha na
kwamba haufanani na binti yao aliyefahamika kwa jina la Ajela Tilifon
mwenye umri wa miaka 16 aliyechukuliwa kijijini hapo tangu mwaka 2012
kwa lengo la kwenda kufanya kazi za ndani mjini Arusha na kwamba baada
ya ndugu kukataa kupokea mwili askari polisi wamewakamata ndugu na
mwaandishi wa habari kwa madai kuwa wanahamasisha vurugu.
Kufatia hali hiyo mkuu wa wilaya ya Muleba Bw.
Lebris Kipuyo alilazimika kufika eneo la vurugu na kuamuru askari polisi
kutawanya wananchi ili magari yaweze kupita na baadaye alifika
hospitali na kuteuwa baadhi ya ndugu,jamaa na wazazi wa mtoto ambao
walikagua mwili wa marehem kisha mkuu wa wilaya akawahutubia wananchi na
kuwataka walioshuhudia mwili waseme ukweli walichokiona nao bila
kusita wamesema maiti inamajeraha tumbo limetobolewa na sehemu za mwili
zimekwaruzika kisha akavishwa nguo na soksi ili kuficha ukweli.
Naye mwaandishi wa habari wa kujitegemea gazeti la
Mwananchi aliyejeruhiwa na askari polisi kwa kupigwa virungu Bw. Shaban
Ndyamkama amesema kuwa yeye ndiye aliyetoa taarifa za vurugu hizo kwa
mkuu wa wilaya ya Muleba baada ya askari kufika eneo la tukio
walimkamata na kumshambulia kwa vipigo kisha wakamshikilia kwa muda hadi
wananchi waliposhinikiza kuachiwa kwake na baada ya waandishi wa
ITV,Radio one kanda ya ziwa kumuomba kamanda wa polisi mkoa wa Kagera
Bw. George Mayunga ambaye amekiri kwa njia ya simu kuwa vurugu hizo
zimesababisha uvunjifu wa amani na kumtaka mkuu wa polisi wilaya ya
Muleba kumuachia huru mwaandishi wa habari ambaye amepelekwa hospitali
na wananchi kwa matibabu zaidi.
Hakuna maoni: