Header ads

Header ads
CLUB MASAI KAHAMA
» »Unlabelled » LOWASSA: SINA MPANGO WA KUSHINDWA, MM SIO FISADI.....MWENYE USHAHIDI ATAJE MAANA SIASA ZA FITINA NA MATUSI ZIMENICHOSHA


Lowassa Akichukua Form ya Urais Dodoma

Lowassa, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisema hana mpango wa kushindwa.

Lowassa aliwasili katika Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma  jana saa 10:20 jioni akiambatana na mkewe, Regina huku akisindikizwa na wabunge mbalimbali pamoja na wanachama wa CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wanachama waliokuwapo katika Ukumbi wa Makao Makuu ya CCM mara baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema hawezi kuzungumzia upande wa kushindwa katika safari yake.

  • “Swali rahisi sana, sina mpango wa kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kama atashindwa katika kinyang’anyoro hicho.


Alipoulizwa kuhusu hali ya nchi kuwa na watu wanaoshambuliwa, Lowassa alisema atajenga Serikali itakayojali utu na uhuru wa vyombo vya habari.

  • “Kwanza nimpe pole yule mwandishi  aliyeteswa. Sikubaliani na mambo ya kuingilia uhuru wa watu kuteswa. Serikali yangu itaheshimu uhuru wa vyombo vya habari,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wanachama wa CCM waliokuwa wamefurika ndani na nje ya ukumbi huo.


Alipoulizwa kwanini anahusishwa na vitendo vya ufisadi, Lowassa aliyekuwa akijibu maswali kwa ufupi, alisema kama kuna mtu ana ushahidi na tuhuma hizo amtaje jina.

  • “Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme, na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi ila tutawapima kwa matendo yao,” alisema.


Kada huyo wa CCM alivitaka vyombo vya habari kutoshabikia tuhuma zisizo na ushahidi, huku akisisitiza kuwa kila mtu apimwe kwa rekodi yake.

Kuhusu uteuzi wa mawaziri, Lowassa hakutaka kulizungumzia akisema bado hajavuka daraja.
“Nitavuka daraja nitakapolifikia,” alisema.

Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alisema ni sera ya CCM iliyotekelezwa baada ya kutokea mgogoro kati ya vyama vya CCM na CUF.

  • “Angalieni kule Marekani, vyama vya Democrat na Republican, vinashindana kwa kura chache sana. Hata sisi tunapishana kwa kura chache, mimi nadhani kama hatupishani sana hivyo hilo ndilo suluhisho,” alisema.



Awali Lowassa aliwashukuru wana CCM waliofurika katika ukumbi huo akisema anajua kero za chama hicho na atakapokuwa rais atazishughulikia.


  • Nawashukuru kwa kunileta nyumbani, nimeitumikia CCM kwa muda mrefu. Nilieleza Dodoma na Arusha nia yangu. Naelewa matatizo wanayopata watumishi wa CCM, nayaelewa. Mishahara midogo, hawakopesheki, hawana fedha za likizo na hawana uchumi mzuri. Wakati wengine wanajengewa nyumba na mikopo wenyewe hawapati,” alisema Lowassa.


Hata hivyo, alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa kuimarisha uchumi ndani ya chama hicho, lakini akasema akiwa rais atafanya zaidi.

  • “Tunaweza kufanya zaidi, tusiwe ombaomba. Nilipokuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini tumejenga jengo la ghorofa 22 Dar es Salaam. Tuna viwanja na maeneo mengi. Nikichaguliwa kuwa rais na mwenyekiti nitaangalia hilo…Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba,” alisema.


Baada ya mkutano huo, Lowassa alikwenda kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma kupata udhamini wa chama hicho ambapo Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi alikuwa miongoni mwa wanachama waliomdhamini, akiwamo mlemavu wa miguu, Idd Omari.

Baadhi ya vigogo waliokuwa ukumbini ni pamoja na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah.

Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Dodoma Mjini baada ya kuchukua fomu, Lowassa alisema vigelele na makofi anavyopigiwa sasa haviwezi kumpeleka Ikulu isipokuwa wananchi wanapaswa kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili iwe njia rahisi ya yeye kuwa mkuu wa nchi.

  • “Naomba watu wajiandikishe, hakikisheni watoto wenu, wajomba na hata washikaji zetu wanajiandikisha katika Daftari la Wapigakura na nitarudi tena kwenu kuomba kura,” alisema.


Huku akishangiliwa na mamia ya wakazi wa Dodoma, Lowassa aliwaambia amekwenda kuomba wadhamini na si kuomba kura, kwani amebanwa na sheria na utaratibu wa chama chao.

Alisema ameguswa na mapokezi waliyompa na kuwashukuru wadhamini wake kwa kumwamini na kusisitiza kuwa atarudi tena kuomba kura.

Leo siombi kura, naweka akiba ya maneno hata wakihesabu nina kampeni potelea mbali, lakini nilipokuwa waziri mkuu nilianza kuijenga Ikulu mnayoiona mpaka leo haijakamilika, nitakuja kuikamilisha, maana yake nini, nahamia Ikulu Dodoma,” alisema mbunge huyo wa Monduli huku akishangiliwa na mamia ya wananchi hao

About Unknown

Kwa jina Naitwa MWEUSI waweza wasiliana nami namba 0757420837, 0629208856 au email: timotheosodoka@gmail.com
«
Next
Chapisho Jipya
»
Previous
Taarifa za zamani

Hakuna maoni:

Leave a Reply