Mifuko ya plastiki inayofungasha
pombe maarufu kama ‘viroba’ imepigwa marufuku na Serikali kuanzia mwakani.
Sambamba na hilo Serikali pia,
imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa
mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliwaambia wanahabari jana sehemu
kubwa ya mifuko hiyo inayotolewa bure imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira
kwa kiasi kikubwa.
Wakati Makamba akiyasema hayo,
Februari mwaka huu,2016 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), Luhaga Mpina aliondoa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki
akisema kuwa itaziweka rehani ajira za Watanzania wanaofanya kazi kwenye viwanda
vinavyotengeneza mifuko hiyo.
Pia, Mpina alisema itapunguza kasi ya
uwekezaji wa viwanda vilivyowekeza katika bidhaa hiyo.
Akizungumza katika siku ya Mazingira
Afrika, Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu alisema maamuzi hayo yamelenga
kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania, tofauti na nchi nyingine
zinazotegemea wazalishaji wa nje ya nchi.
Makamba akizungumzia uamuzi mpya wa
kuzuia mifuko ya plastiki, alisema matumizi ya mifuko inayofungashia vileo na
inayotumika katika matumizi mengine husambaa na kuchafua mazingira. Alisema
mifuko ya plastiki inatajwa kuziba mifereji na kusababisha mafuriko na athari
nyingine za mazingira.
“Leo (Jana), tumeamua kutangaza ili
kuwaanda wahusika wasiendelee kuwekeza katika mifuko hii badala yake wasubiri utaratibu
mwingine utakaowekwa na Serikali,” alisema Makamba na kuongeza kuwa:
“Asilimia kubwa ya uchafu kwenye nyanzo vya
maji, mito, maziwa na fukwe za bahari ni mifuko ya plastiki.”
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa
Bumbuli, alisema Serikali inakamilisha majadiliano ya ndani na baadaye
itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku ya moja kwa moja mifuko
hiyo.
Alifafanua kwamba Serikali itatoa
muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko hiyo ili
kujiandaa kuacha shughuli hizo na badala yake itawezesha mazingira ya
utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.
“Kwa wanaotengeza mifuko hii na
kuiuza katika soko la nje hatuna tatizo nao waendelee. Ila kwa soko la ndani
hawataruhusiwa kufanya hivyo.Zuio hili litakuwa la kisheria siyo kwa maneno,”
alisisitiza Makamba.
Aliongeza kuwa katika kuonyesha
Serikali imedhamiria kupambana na hali hiyo wizara yake imeamua kutuma timu ya
watu watano kwenda Rwanda kujifunza namna bora ya kudhibiti matumizi na kuzuia
mifuko hiyo tangu mwaka 2008.
Waziri huyo alitoa wito kwa
watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko hiyo kujiandaa na zuio hilo
na katika siku zijazo Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya
kuanza zuio huku taratibu nyingine za kina zikifuata ili kuondoa mkanganyiko.
Katika hatua nyingine, Makamba alisema
maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5
kila mwaka hayatafanyika kitaifa badala yake wizara imewaelekeza wakuu wa mikoa
kufanya maadhimisho katika maeneo yao.
“Tumewapa miongozo kuhusu utekezezaji wa
shughuli hizo za maadhimisho zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira
hususan nyanzo ya maji amabayo ni muhimu kwa viumbe hai,” alisema Makamba.
Kwa mujibu wa Makamba, kauli mbiu ya
mwaka huu kitaifa juu ya maadhimisho hayo ni ‘ tuhifadhi vyanzo vya maji kwa
uhai wa taifa letu’aliwashauri na kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kupanda
miti, kudhibiti uchomaji wa misitu
Ofisa Mwandamizi Mazingira wa Nemc,
Arnold Kisagala alisema nusu ya mifuko ya plastiki nchini inazalishwa na
kuingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya.
Alisema agizo la Waziri Makamba
litawezekana, lakini linahitaji ushirikiano kutoka kwenye sekta zingine kwa
kuwa viwanda vingi vya mifuko ya plastiki vipo Kenya.
Hakuna maoni: