Sakata
la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka fedha katika akaunti maalumu
kwenye benki za biashara limechukua sura mpya baada ya Gavana wa Benki
Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kusema si kosa kisheria.
Profesa
Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRA iliyovunjwa na Rais
John Magufuli Jumapili iliyopita, alisema mjini Arusa jana kuwa hakuna
hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum isipokuwa hilo suala
lilikuwa na hali nyingine.
Japokuwa
Profesa Ndulu hakutaka kufafanua zaidi kwa maelezo lilichomekewa tu
katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea hali ya uchumi,
alisema hali hiyo ndiyo suala lililozungumzwa na siyo kusema “fixed
deposit account” ni mbaya.
“Kwani
amesema fixed account zote ni mbaya, pamoja na za watu binafsi? Ndo
hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa hiyo nilikuwa tayari,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa
Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari
walipotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka fedha
kwenye akaunti maalumu tena benki binafsi.
Kauli
hii ya Profesa Ndulu imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kueleza
kilichochangia kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi,
Bernard Mchomvu na pia kuivunja bodi yake iliyokuwa na wajumbe tisa.
Kati ya wajumbe hao tisa, watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na wanne
ni wa kuteuliwa.
Wajumbe
wanaoingia kwenye Bodi kwa mujibu wa sheria ni Gavana wa BoT, Profesa
Beno Ndulu; Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata; Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Doto James; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
Zanzibar, Khamis Mussa Khamis; na Katibu Mkuu Mipango. Bodi hiyo
ilivunjwa Jumapili iliyopita.
Rais
Magufuli alisema juzi kuwa Bodi ya TRA iliyokuwa na watendaji hao wakuu
wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi
wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.
“Juzi
hapa tumekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya
matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit
account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela
nikazichukua na bodi kwaheri,” alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni
rasmi kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
yaliyofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambako jumla ya watu 4038
walihitimu shahada mbalimbali
Ukwasi wa mabenki
Katika
hatua nyingine Profesa Ndulu amesema ukwasi wa fedha katika mabenki
umeshuka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma hatua inayotatiza utoaji wa
mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari mara baada ya kufungwa mkutano wa 18 wa
taasisi za fedha uliofanyika kwa siku mbili jijini Arusha alisema hali
hiyo inafanyiwa kazi na wadau wa taasisi hizo ili kuja na mbinu kufanya
kuwa endelevu kwani uchumi unategemea uwekezaji unaotegemea mikopo ya
muda mrefu.
Profesa
Ndulu alisema BoT itahakikisha inaziwezesha benki kuendelea na jukumu
lao la kutoa mikopo pia kuwa wabunifu wa kutafuta pesa kwa ajli ya amana
badala ya kutegemea Serikali pekee.
“Benki
zinaweza kukusanya amana kwa kiwango kikubwa lakini kama nilivyosema
jana (juzi) kuwa katika kila Sh60 kati ya Sh100 zipo kwenye mikono ya
watu badala ya kuwekwa akiba benki hivyo ni muhimu zikawekwa mbinu ya
kuzipata kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji kuzitumia kwenye
uzalishaji,” alisema.
Alisema
katika kufanikisha mpango huo lazima kuvutia mitaji kutoka nje kwani
hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kupiga hatua kwa kutegemea fedha za
maendeleo na uwekezaji zitokane na mapato ya ndani pekee akitolea mfano
wa China kuwa ni mfano uchumi wake kutegemea mitaji inayotoka nje ya
nchi hiyo.
Katika
hatua nyingine Profesa Ndulu alisema amekubaliana na wadau wa sekta ya
fedha kuongeza nguvu katika kutoa mikopo na kuboresha mifumo ya taarifa
kwa wale wanaotaka mikopo kwa ajili ya kilimo katika mnyororo mzima wa
thamani kuanzia uzalishaji hadi kufika kwenye soko.
Profesa
Ndulu alisema Tanzania imekaa vizuri kijiografia kufanya biashara na
nchi zisizo na bahari zikiwemo Malawi, Uganda, DRC na Zambia katika
kuwezesha sekta ya fedha kusaidia eneo la usafirishaji, bandari kufanya
kazi na huduma kutolewa inavyotakiwa.
Mwenyekiti
wa wenye mabenki ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk Charles
Kimei amesema waendeshaji wa mabenki wamenufaika na kuelewa mikakati na
fursa za Serikali ambayo itawawezesha wao kutoa fedha kwa
wafanyabishara.
Alisema
wao kama CRDB wameweza kukusanya amana za Sh500 bilioni zinazokopeshwa
kwa wafanyabiashara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na
kufungua matawi madogo madogo 100 nchi nzima.
Dk
Kimei alisema serikali inapobanwa kifedha kutokana na kutegemea
mashirika ya umma inawapa fursa sekta binafsi kupanua wigo wao kuwafikia
wananchi wengi.
Hakuna maoni: