Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule
ya Sekondari Gerezani, Shakil Sures amelazwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi na polisi kwenye
mazingira ya kutatanisha.
Tukio hilo lililotokea Jumatatu eneo la Fire, Upanga licha ya watu
kusikia milio ya risasi, kushuhudia polisi wakipita na kumuona kijana
huyo akiwa tayari kajeruhiwa, lakini hakuna mwenye maelezo sahihi kuhusu
nini kilitokea hadi askari hao wakachukua hatua hiyo.
Baadhi ya waliokuwapo eneo la tukio siku hiyo walidai kuwaona askari
waliokuwa eneo hilo wakirusha risasi, bila kujua walikuwa wakipambana na
nani.
Mmoja wa mashuhuda, Athumani Simba alidai walidhani ni majibizano ya
risasi kati ya askari na majambazi, baada ya kuona gari la polisi
likipita eneo hilo.
“Niliwaona askari wawili wakielekea eneo la Fire huku wakipiga risasi,
ghafla nilimuona mwanafunzi akilia huku akiwa ameshika mguu wake akiomba
msaada,” alisema Simba.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema mwanafunzi huyo
alifikishwa hospitalini hapo jioni ya Jumatatu na kwamba jeraha lake
linaendelea vizuri.
“Tumempokea mwanafunzi Shakil juzi jioni na kidonda chake kimesafishwa na kinaendelea vizuri,” alisema Aligaesha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Hamduni Salum alisema upelelezi kuhusu
tukio hilo unaendelea. Hata hivyo, hakueleza mazingira ya tukio lenyewe
yalivyokuwa.
“Tunawashikilia askari polisi wawili waliokuwa zamu siku hiyo ya tukio,
upelelezi unaendelea ili kuangalia kwa nini walitumia nguvu kubwa kiasi
hicho,” alisema Kamanda Salum.
Hakuna maoni: