MWALIMU Mkuu wa Shule ya Sekondari
Ridhwaa Seminary iliyopo wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Yusuph
Kivugo, amemshambulia mwanafunzi wake, Mbaraka Mwalimu, kwa kumpiga
ngumi usoni na kumsababishia maumivu makali.
Mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha nne
katika shule hiyo iliyopo Kinondoni Mkwajuni, alikutwa na mkasa huo
Novemba 3, mwaka huu wakati akijiandaa na mtihani wa Historia.
Kwa mujibu wa ratiba ya mitihani ya
taifa ya kidato cha nne inayoendelea nchini, mtihani huo ulikuwa
unafanyika mchana, lakini hata hivyo hakufanya kutokana na maumivu
aliyokuwa nayo.
“Tulikuwa msikitini na wenzangu
tunasoma, ilikuwa ni saa mbili asubuhi kabla ya mtihani wa Historia
kuanza, mwalimu alikuja akauliza kwanini tunapiga kelele na kuanza
kutupiga.
“Upande wa pili kulikuwa na wanafunzi wa
pre-form one ndio waliokuwa wakipiga kelele, nilishangaa kamkunja
mwenzangu anaitwa Mohamed akawa anampiga mangumi, mimi nilijua labda
kuna kosa amefanya.
“Katika kujitetea akina Mudy walikimbia,
mara akaja kwangu akanishika akaanza kunishambulia, amenipiga ngumi
nyingi za usoni, kwenye taya na nyingine jichoni kiasi kwamba sikuweza
kufanya mtihani kwani jicho lilivimba sana,” alisema.
Mwalimu wa nidhamu shuleni hapo, Omary Ikome, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema jukumu lake ni kusimamia nidhamu kwa wanafunzi na kwamba suala hilo lipo juu ya uwezo wake.
“Nilimkuta Mbaraka analia na jicho la
kushoto limevimba, nilimuuliza akasema amepigwa na mkuu. Mimi nasimamia
nidhamu kwa wanafunzi, lakini kwa kuwa kitendo hiki kimefanywa na bosi
wangu, siwezi kuzungumzia zaidi kwani lipo juu ya uwezo wangu,” alisema.
Mwalimu mkuu huyo alipoulizwa kiini cha tatizo, hakuweza kutoa ushirikiano na kumfukuza mwandishi ofisini kwake.
Chanzo-Mtanzania
Hakuna maoni: