Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuona Askofu wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima anayekabiliwa na kesi ya kushindwa
kuhifadhi silaha, ana kesi ya kujibu.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alitoa uamuzi huo jana
baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri pamoja na
vielelezo.
Alisema
kutokana na ushahidi huo, ameona upande wa Jamhuri umejenga kesi hivyo
Gwajima na wenzake watatu, wana haki ya kujitetea, kuita mashahidi au
kukaa kimya.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai kuwa washtakiwa watajitetea kwa njia ya kiapo na watakuwa na mashahidi watatu.
Hakimu
Mkeha alisema Desemba 13, mwaka huu, washtakiwa watajitetea na siku
hiyo atasikiliza utetezi wa washtakiwa wote wanne pamoja na mashahidi
wao.
Mbali
na Gwajima, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni msaidizi wa askofu
huyo, Yekonia Bihagaze (39), mfanyabiashara George Mnzava (43) na mkazi
wa Kimara Baruti, Geoffrey Milulu (31).
Inadaiwa
kuwa, Machi 29 mwaka jana, katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A,
washitakiwa walikutwa wakimiliki bastola aina ya Baretta yenye namba
CAT 8802 bila kuwa na kibali kutoka mamlaka inayohusika na silaha na
milipuko.
Aidha,
inadaiwa washtakiwa hao walikuwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu
za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya shotgun. Gwajima
anadaiwa kushindwa kuhifadhi silaha katika hali ya usalama.
Hakuna maoni: