Fundi wa kuziba pancha, Harson Solomon (38), mkazi wa wilayani hapa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kupatikana na misokoto 601 ya bangi.
Kifungo
hicho kimeangukia sheria mpya ya udhibiti wa dawa za kulevya
iliyosainiwa Mei 11, 2015 na aliyekuwa Rais wakati huo, Jakaya Kikwete.
Imeelezwa Solomon ni miongoni mwa washtakiwa wa mwanzo kufungwa kwa
sheria hiyo.
Awali,
sheria ilikuwa inatoa mwanya wa faini na mtu anaposhindwa kulipa ndipo
hutumikia kifungo jela lakini hivi sasa anayepatikana na hatia ya
kukutwa na kiwango kikubwa hutupwa jela.
Kifungu
cha 11(1) D cha sheria hiyo mpya, kinaeleza wazi mtu anayezalisha,
kumiliki, kuuza, kununua au kusafirisha dawa za kulevya ikiwamo bangi,
adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Joachim Tiganga baada ya
kuridhishwa bila kuacha shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Wakili
wa Serikali, Ignas Mwinuka alidai kortini kuwa Desemba 1, 2015 katika
maeneo ya Mwika Kimangara, Moshi Vijijini mshitakiwa alipatikana na
kiasi hicho cha bangi.
Pia, anadaiwa kuruhusu eneo lake kutumika kuuza bangi na gongo.
Akisoma
hukumu, Hakimu Tiganga alisema matumizi ya dawa za kulevya yanazidi
kuongezeka nchini na kuathiri jamii, hivyo Mahakama inatoa adhabu hiyo
iwe fundisho kwa wengine.
Katika
kipindi chote tangu afikishwe kortini kwa mara ya kwanza Desemba 11
mwaka jana, mshtakiwa alikana mashtaka hadi alipotiwa hatiani na
kuhukumiwa jana.
Hakuna maoni: