MANUSURA wa ajali ya jahazi namba Z5512 MV Burudani iliyotokea usiku wa
kuamkia jana na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 12 na majeruhi zaidi
ya 33, wameeleza kuwa chombo hicho kilipigwa na upepo mkali baharini na
kukosa mwelekeo kisha kukatika vipande.
“Baada ya kuondoka bandarini nahodha pamoja na wasaidizi wake
walilazimika kusimamisha chombo kwa takribani saa mbili hivi ili kupisha
upepo na baadaye tukaondoka, lakini hatukufika mbali chombo kikapigwa
na wimbi na kupoteza mwelekeo ambapo baadaye kikajaa maji na kukatika
katikati, “ alisema Emmanuel Mniga, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo,
mkazi wa mkoa wa Morogoro, ambaye amelazwa katika wodi ya A1 katika
Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Tanga.
Katika ajali hiyo, miili zaidi ya 12 ya baadhi ya abiria waliokufa maji
katika jahazi hilo maarufu kwa jina la Sayari, lililokuwa likisafiri
kutoka jijini Tanga kwenda mkoa wa Kaskazini Pemba, iliopolewa na
imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo ya Bombo.
Aidha abiria wengine zaidi ya 33 waliojeruhiwa, wamelazwa katika
hospitali hiyo, ambapo wawili kati yao wanaendelea na matibabu chini ya
uangalizi maalumu. Kati ya majeruhi hao, wamo watu wazima sita (6) na
watoto sita (6) waliokuwa wakisafiri pamoja na wazazi wao katika chombo
hicho, ambacho mpaka jana mchana idadi kamili ya abiria waliokuwemo
haijafahamika.
Ilielezwa kuwa baadhi ya wakazi walioliona jahazi hilo kabla ya kuanza
safari, walidai lilikuwa limebeba shehena ya mzigo ambao ni bidhaa
mbalimbali ikiwemo pumba, maharage, vinywaji aina ya bia na abiria zaidi
ya 50 wakiwemo watu wazima pamoja na watoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alithibitisha tukio
hilo na kusema walipokea taarifa za kupatikana kwa miili ya baadhi ya
abiria hao jana saa 12.30 asubuhi na kuanza kufuatilia.
“Ajali ilitokea saa 7.30 usiku wa kuamkia jana na taarifa za awali
zinaonesha chanzo cha ajali hiyo ni dhoruba kali,” alisema. Aliongeza,
“Tulipata taarifa ya kuzama majini kwa chombo hicho cha mv Burudani
maarufu kama Sayari kinachomilikiwa na mkazi mmoja wa Pemba
aliyetambulika kwa jina moja la Suleiman maarufu Bwimbwi..... Chombo
hicho kilitokea bandari isiyo rasmi (bubu) eneo la Sahare hapa jijini
Tanga kuelekea Kaskazini Pemba na ndipo kikakutwa na ajali hiyo, “
alisema.
Kamanda Wakulyamba alisema pamoja na kupatikana majeruhi na miili hiyo,
Polisi kwa kushirikiana na majeshi ya Wanamaji, Zimamoto na Uokoaji na
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanga bado wanaendeleza jitihada za
kutafuta abiria wengine kwasababu idadi yao bado haijajulikana.
“Tatizo lililopo ni kwamba idadi kubwa ya vyombo vinavyosafirisha abiria
na mizigo kati ya Tanga na Pemba havina mifumo rasmi ya utambuzi pamoja
na ile ya mawasiliano ambayo ingeweza kutumika kurahisisha mawasiliano
baina ya walioko chomboni na wenzao walioko nchi kavu wakati wa safari
ili kusaidia kufanya mawasiliano hasa wakati inapotokea ajali kama hii,
“alisema.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga ya
Bombo, Dk Goodluck Mbwilo akizungumza jana mchana katika mahojiano nje
ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo alikiri kupokea miili
12 pamoja na majeruhi 33.
“Majira ya saa nne jana asubuhi ndipo tulianza kupokea maiti pamoja na
majeruhi ambao 33 tumewalaza katika wodi zetu za A 1 na A2 wakiendelea
na matibabu... na tayari hapa tumeanza kuruhusu wananchi ili waje
kutambua marehemu”, alisema.
Kwa upande wake, muuguzi wa zamu katika wodi ya A2, Judith Mzia
alimweleza mwandishi kwamba amepokea jumla ya majeruhi 17 kati yao
wakiwemo watoto watatu na wanawake watu wazima.
“Majeruhi 15 wanaendeleza vizuri baada ya kupata huduma lakini wawili
kati yao hali za afya zao hazijaimarika inaonekana walikunywa maji mengi
hivyo wapo katika uangalizi maalumu na hapa kama unavyoona mmoja wao
ndio tunajaribu kumwekea hewa ya oksijeni, “ alisema.
Baadhi ya majeruhi wasimulia mkasa Mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, Juma
Maduhu ambaye amelazwa wodi ya A1 alisema, “Baada ya kuwasili hapa Tanga
tukitokea Bariadi mimi na wenzangu wawili.
Tulianza safari yetu kuelekea Pemba kwa jahazi hiyo saa 5 usiku nikiwa
nimeambatana na ndugu zangu, Joji Nindwa na John Kombo na baada ya muda
majira ya saa 7.30 usiku, ndipo tulipokumbwa na ajali hii ila namshukuru
sana Mungu kwa sababu ndugu zangu wote nimewaona wapo salama, “alisema.
Mariam Idi, mkazi wa Moa wilayani Mkinga, ambaye amelazwa wodi ya A1
alisema katika safari yake hiyo, waliambatana na ndugu zake watano wa
familia moja.
“Tulikuwa watu wazima wawili ambapo mwenzangu anaitwa Halima pamoja na
watoto wetu watatu sasa ilipofikia saa 7.30 usiku kulikuwa na upepo
mkali ambao ulisabisha chombo kuyumba na kujaa maji na ndipo katika
kujitetea tumeokoka watu wanne lakini mtoto wetu mmoja aitwae Sefu
Abdala mwenye umri wa miaka minne hajapatikana,” alisema.
Majeruhi mwingine, Emmanuel Mniga mkazi wa mkoani Morogoro, ambaye
amelazwa katika wodi ya A1, alisema alipanda jahazi hilo kwa lengo la
kupelekwa biashara Pemba ambayo hata hivyo hakuweza kuitaja.
“Baada ya kuondoka bandarini nahodha pamoja na wasaidizi wake
alilazimika kisimamisha chombo kwa takribani saa mbili hivi ili kupisha
upepo na baadae tukaondoka lakini hatukufika mbali chombo kikapigwa na
wimbi na kupoteza mwelekeo ambapo baadae kikajaa maji na kukatika
katikati, “ alisema Mniga.
Aliongeza, “Mimi nilijiokoa kwa kushikilia kamba ngumu ambayo ilikuwa
imefungia sehemu ya turubai katika chombo hicho hadi nilipookolewa...Kwa
kweli namshukuru Mungu, “alisema.
Hata hivyo, mmoja wa wakazi aliyejitambulisha kama Hamadi Ali Hamadi,
mkazi wa Sahare Kijijini, alimweleza mwandishi wetu kwamba yeye ni ndugu
wa karibu wa nahodha wa jahazi hilo, Badru Mohamed alidai kwamba ajali
ilitokea katika mwamba wa Nyuli katika Bahari ya Hindi jijini Tanga.
Alisema, “Jana usiku wa saa sita nilishuka bandarini Sahare kukagua
jahazi hiyo kabla ya kuanza safari yake ambapo nilikuta ikiwa na abiria
32, gunia 20 za pumba, maharage kilo 60 ambazo zilikuwa zimefungashwa
katika polo 25 pamoja na masanduku (kreti) 100 za vinywaji aina ya
bia...kwenye safari hiyo ndugu zangu walikuwa jumla yao ni wanne, “
alisema.
“Nimepita kukagua miili nimebaini mwili wa nahodha kwamba ni mmoja wa
marehemu lakini ndugu zangu wengine watatu wote wapo hai...
Nilipozungumza nao wamenieleza kwamba marehemu Badru (nahodha wa chombo )
aliondoka akiwa na mabaharia (wasaidizi) wake wanne ambao binafsi
siwafahamu kwa majina ambapo inasemekana dhoruba ndiyo ilipiga chombo na
kukatika katikati, “ alisema.
Hata hivyo, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu
na Majini mkoa wa Tanga, alisema atatoa taarifa rasmi leo kwa vyombo
vya habari kuhusu ajali hiyo.
Wakati huo huo, Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela kwa vifo vya watu 12 vilivyosababishwa
na kuzama kwa jahazi waliyokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda Pemba.
Katika salamu zake, Rais alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia
jana katika kisiwa cha Jambe kilichopo katika Bahari ya Hindi umbali
mfupi kutoka Tanga mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao watu
wengine 33 wamenusurika na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya
Bombo Mkoani Tanga.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya watanzania wenzetu
waliopoteza maisha katika ajali hii ya kuzama jahazi, tumepoteza
wapendwa wetu, watoto wetu na watu wazima ambao kwa hakika familia zao
ziliwategemea katika maisha ya kila siku, nakuomba Mkuu wa Mkoa
unifikishie pole nyingi kwa familia za marehemu wote na jamaa zao,”
alisema Rais Magufuli katika salamu hizo za pole, zilizotolewa jana na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, Rais amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na
pia amewataka wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na
subira katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao.
Magufuli pia amewatakia matibabu mema majeruhi wote, walionusurika
katika ajali hiyo ili wapone haraka, warejee katika familia zao na
waendelee na ujenzi wa Taifa.
Hakuna maoni: