Ikiwa ni siku moja toka biashara ya filamu ‘feki’ za nje zipigwe
marufuku mpaka pale wafanyabiashara wa filamu hizo watakapokamilisha
taratibu za ulipaji wa kodi, mengi yameendelea kuibuka, ikiwa ni pamoja
na wasanii ambao walihusika kwenye kampeni hiyo kuambiwa wanatumika
kisisasa.
Wasanii hao wakiongozwa na JB, Jumatano hii waliungana na ofisi ya Mkoa
wa Dar es salaam kufanya opesheni hiyo ndani ya soko la Kariakoo kwa
madai filamu hizo zinawanyonya wasanii wa filamu wa ndani kwa kuwa
zinauzwa bila kulipiwa kodi wakati wao filamu zao zinalipiwa kodi.
JB amedai amesikitishwa kuona baadhi ya watu wanalihusisha tukio hilo na siasa.
“Ndugu zangu kuna jambo naomba niongee na nyinyi, hivi mnajua
tunayoyalilia ni maisha yetu, kwa nini kila kitu mnahusisha na siasa?
Hivi ni haki mimi nitozwe 30% ya pato langu mwingine asitozwe?,”
aliandika JB Instagram.
“Kwenye shida mimi sitajali nani ananisaidia ilimradi anagusa maslahi
yangu, ugali wangu, ninakiri sinema zetu zina mapungufu mengi lakini
hiyo siyo sababu za kuacha kudai haki zetu. Ni kama mgonjwa akiumwa leo
anapelekwa kwa mganga kesho anapelekwa kuombewa anatetea roho yake.
Nawaomba sana hatukatai mkitusema kuwa movie zetu zina matatizo lakini
ngoja tumalize hili, tusichanganye, na pia hakuna aliye sema zifungiwe
hapana zifate utaratibu kama sisi tunavyo fata. Hizo hizo movie zetu
mbovu ndio zinatuwezesha kuishi,” aliongeza.
“Lakini pia lazima mfahamu biashara hii ni kubwa kuliko mnavyodhania,
movie 2 zinanitosha kuishi kwa mwaka mzima, ushawaza ni kiasi gani mimi
pamoja na kushiriki mapambano haya ni kama nimemaliza muda wangu kwenye
kazi hii nimebakiza movie 1 tu. Je udhani mwanao au ndugu yako naye
anaweza kuingia huku?. Tukiiponda tasnia huniharibii mimi tu, unaharibu
maisha ya watu wengi wajao ambao watafanya vizuri zaidi yetu,”
alifafanua zaidi.
Sakata hili limewagawa wasanii wa filamu nchini mara mbili. Wapo ambao
wanaamini njia hiyo itasaidia kukuza tasnia ya filamu huku wengine
wakipinga njia hiyo kwa madai kua siyo sahihi kwani filamu za nje
zilikuwa nchini toka zamani.
Hakuna maoni: