Askari polisi
wakiweka kwenye gari la polisi mwili wa Mwenyekiti wa chama cha
waendesha pikipiki manispaa ya Shinyanga Jacob Paul aliyejiua leo Juni
10,2017 kwa kujinyonga nyumbani kwake huku chanzo kikihusishwa na
mgogoro wa waendesha bodaboda na jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga.
Mamia ya wakazi wa Shinyanga wamepigwa
butwaa baada ya mwenyekiti wa chama cha waendesha pikipiki maarufu
bodaboda katika manispaa ya Shinyanga Jacob Paul (36) kujiua kwa
kujinyonga kwa kutumia waya wa simu chumbani kwake. Mwandishi mkuu wa
Malunde1 blog,Kadama Malunde anaripoti.
Tukio hilo la kushangaza limetokea
Jumamosi Juni 10,2017 majira ya saa nane mchana katika mtaa wa Mwinamila
kata ya Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema Jacob
Paul ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma alifika nyumbani kwake leo
majira ya saa saba mchana akiwa amepakizwa kwenye pikipiki na mwendesha
bodaboda mwenzake huku akionekana kuwa mtu mwenye furaha kisha akaingia
ndani kwake.
Walieleza kuwa baada ya takribani dakika
30 watoto wawili marehemu walifika nyumbani wakitaka kuingia ndani ya
nyumba lakini mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani walijaribu kumuita
lakini hakujibu ndipo wakaamua kwenda kuchungulia dirishani.
Walifafanua kuwa watoto hao
walipochungulia dirishani walimuona baba yao akiwa amening’inia chumbani
kisha kutoa taarifa kwa majirani na baba mwenye nyumba akaamua kutoa
taarifa kwa jeshi la polisi.
“Mke wa
marehemu hakuwepo tulipoona kuwa mlango ni mgumu kufunguka tuliamua
kuuvunja na kumkuta amejiua na huenda chanzo cha kifo chake kimetokana
na msongo wa mawazo kwa sababu tangu kutokea kwa tukio la mwendesha
bodaboda Joel Gabriel Mamla (26) kufariki dunia,alikuwa anasema
waendesha bodaboda wenzake wamekuwa wakimlalamikia kuwa anashirikiana na
polisi kukamata waendesha bodaboda waliofanya vurugu hivi karibuni”,alieleza jirani Sarah Edward.
“Jana
alikuwa anasema kuwa anapewa vitisho na wenzie kuwa anawasaliti na
kusababisha waendesha wakamatwe na polisi na pikipiki zao”,alieleza jirani huyo.
“Nilikwambia
mme wangu ujiuzulu uenyekiti,ona sasa waendesha bodaboda wenzako
wamekuponza,wamekusababishe ujiue baba Joshua,umeacha familia yako
bora,watoto hawa watalelewa na nani”, mke wa marehemu Rebeca Amos aliyekuwa analia muda wote wakati wa tukio alisikika akiongea kwa uchungu.
Alisema mme wake amekuwa akipokea vitisho kwa watu wasiojulikana wakimtuhumu kuwasaliti na kusababisha wakamatwe.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema
kuwa marehemu alikuwa analalamikiwa na waendesha bodaboda wenzake kuwa
anashirikiana na jeshi la polisi kugandamiza waendesha bodaboda wenzake.
“Mwenyekiti anadaiwa kuwasaliti
wenzake,hata kipindi kile mwendesha bodaboda Boaz William aliyefariki
dunia kwa kugongwa gari wakati akidaiwa kuwakimbia askari wa usalama
barabarani mjini Shinyanga anadaiwa kushirikiana na polisi kutorosha
mwili wa marehemu na kuupeleka Kigoma kwa ajili ya mazishi ambapo hata
waendesha bodaboda hawakupata hata nafasi ya kuaga mwili wa
marehemu”, .
Diwani wa kata ya Ngokolo,Emmanuel Ntobi
alifika eneo la tukio alimuomba rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli kuunda tume huru ya kijaji kuchunguza vifo vya
waendesha bodaboda katika manispaa ya Shinyanga.
“Sasa
idadi ya vifo vya waendesha bodaboda vimetokea Shinyanga,kuna utata
kwani jamii inasema vifo vinasababishwa na askari polisi huku jeshi la
polisi nalo likidai waendesha bodaboda ndiyo wanasababisha vifo vyao kwa
kukiuka sheria za usalama barabarani,mpaka sasa pikipiki nyingi
zimekamatwa”,alieleza Ntobi.
Kamanda wa jeshi la polisi ACP Muliro
Jumanne Muliro aliyekuwepo eneo la tukio alisema wamekuta mwenyekiti
huyo wa waendesha bodaboda amejinyonga kwa kutumia waya mgumu wa simu
katika chumba chake.
“Tumepata taarifa kuhusu tukio
hili,tulipofika tumekuta amefariki kwa kujing’iniza kwa waya,tumeuchua
mwili wa marehemu kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi hospitalini,sisi kazi
yetu ni kuchunguza chanzo cha kifo,bado tunafanya uchunguzi zaidi juu
ya tukio hili tutatoa taarifa zaidi baadaye”,alisema kamanda Muliro.
Tukio la mwenyekiti wa waendesha
bodaboda kujiua limetokea siku tano tu baada ya jeshi la polisi mkoani
Shinyanga,kulazimika kuwapiga mabomu ya machozi waendesha bodaboda, kwa
kitendo cha kuundamana kupinga kifo cha mwenzao Joel Gabriel Mamla
(26),kilichodaiwa kusababishwa na askari polisi PC Edmund baada ya
kumkamata kwa kosa la kutovaa helmet. SOMA <<HAPA>>
Kwa mujibu wa jeshi la polisi watu 26
walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Shinyanga kwa mashtaka ya
kufanya mkusanyiko usio halali,kufanya fujo na kujaribu kufanya
maandamano kinyume na sheria.
Kati yao David Laurent alikiri kosa lake
na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela na wengine kesi yao
iliahirishwa na itaendelea Julai 23,2017.
HII HAPA TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUHUSU WAENDESHA BODABODA KUFIKISHWA MAHAKAMANI.
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA SHINYANGA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 10/06/2017
TAREHE 09/06/2017 WATU 26 WALIFIKISHhWA
KATIKA MAHAKAMA YA WILAYA YA SHINYANGA NA KUFUNGULIWA KESI YA JINAI NO
134 NA BAADAE KUSOMEWA MASHITAKA YA KUFANYA MKUSANYIKO USIOHALALI ,
KUFANYA FUJO NA KUJARIBU KUFANYA MAANDAMANO KINYUME NA SHERIA.
MAKOSA HAYO WALIYATENDA TAREHE
07/06/2017 MAJIRA YA SAA 04.30 ASUBUHI WAKATI KUNDI LA WATU WAPATAO 80
WENGI WAO WAKIWA NI WAENDESHA PIKIPIKI MAARUFU KAMA BODABODA WAKIWA ENEO
LA IBINZAMATA MANISPAA YA SHINYANGA KWA PAMOJA WALIKUSANYIKA WAKAPANGA
NA KUFANYA MAANDAMANO KINYUME NA SHERIA NA KUANZA KUYARUSHIA MAWE BAADHI
YA MAGARI NA KUSABABISHA USUMBUFU KWA BAADHI YA RAIA NA WATUMIAJI
WENGINE WA BARABARA NA HIVYO KUJENGA HOFU NA KUPELEKEA KUVUNJIKA KWA
AMANI KATIKA ENEO HILO.
MTUHUMIWA MMOJA NO 18 KATIKA HATI HIYO
YA MASHITAKA AITWAYE DAVID LAURENT ALIKIRI KOSA LAKE BAADA YA KUSOMEWA
MASHTAKA HAYO NA MWANASHERIA WA SERIKALI CAROLINE MUSHI MBELE YA HAKIMU
DENIS LUWUNGO.
MTUHUMIWA HUYO AMEHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIEZI SITA JELA NA WENGINE KESI YAO IMEAHIRISHWA NA ITAENDELEA TAREHE 23/06/2017.
WAKATI HUOHUO IMETOKEA AJALI YA PIKIPIKI
NA KUSABABISHA KIFO. TAREHE 10/06/2017 SAA 08 USIKU BARABARA YA MAGANZO
ENEO LA MATANDA SISI KWA SISI ZONE 1 MWENDESHA PIKIPIKI SHINJE MACHIYA
MKAZI WA BUGWETO AKIWA NA PIKIPIKI NO MC 303 HUKU AKIIENDESHA KWA KASI
NA BILA KUWA NA KOFIA NGUMU HELMET ALIPATA AJALI BAADA YA KUANGUKA NA
KUFARIKI PALEPALE BAADA YA KUVUJA DAMU NYINGI KICHWANI.
CHANZO CHA KIFO HICHO NI MWENDO KASI ,
KUTOVAA HELMET NA KUPELEKEA AJALI ILIYOSABABISHA KUVUJA KWA DAMU NYINGI
KICHWANI NA HATIMAYE KUFA. MWILI WA MAREHEMU UMEHIFADHIWA HOSPITALI YA
RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA.
IMETOLEWA NA MULIRO J MULIRO (ACP) - RPC SHINYANGA.
Angalia picha hapa chini
Kamanda wa jeshi la polisi ACP Muliro Jumanne Muliro (wa tatu kutoka kushoto) akiwa nyumbani kwa marehemu Jacob Paul
Wananchi wakiwa nyumbani kwa marehemu Jacob Paul
Kamanda wa jeshi la polisi ACP Muliro Jumanne Muliro akisikiliza maelezo kutoka kwa mke wa marehemu,bi Rebeca Amos
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa
Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akielekea kwenye chumba cha marehemu
Jacob Paul akiwa ameambatana na maafisa wa jeshi la polisi huku ulinzi
ukiwa umeimarishwa
Askari polisi wakiimarisha ulinzi nyumbani kwa marehemu Jacob Paul
Mke wa marehemu akilia kwa uchungu wa kupoteza mme
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Wananchi wakiwa nyumbani kwa marehemu Jacob Paul
Askari polisi wakiwa wamebeba mwili wa marehemu Jacob Paul
Askari polisi wakiwa wamebeba mwili wa marehemu
Mwili wa marehemu ukiwekwa kwenye gari la polisi
Askari polisi wakiondoka na mwili wa marehemu
Jirani yake na marehemu,Sarah Edward akielezea tukio hilo
Diwani wa kata ya Ngokolo Emmanuel Ntobi
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la mwenyekiti wa
waendesha bodaboda manispaa ya Shinyanga,Jacob Paul aliyejiua kwa
kujinyonga TANGAZA NASI KUPITIA kahamayetu@gmail.com sim 0763 288 300
Hakuna maoni: