Kwa maneno ya siku hizi ni kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Jaji Fredrick Werema ‘amelikoroga na kulinywa mwenyewe’, baada ya jana
kutoa kauli ya kuudhi alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali
lake visiwani humo, iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na
kutoka.
Kauli iliyoonyesha kuwagawa wabunge katika mafungu mawili; wa bara na
Zanzibar, ilimlazimu Jaji Werema baadaye kusimama bungeni na
kuwaangukia akiwaomba radhi waliokerwa na kauli yake na pia kuliomba
radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda na wananchi.
Kuondoka kwa wabunge hao kulitokana na mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mbarouk Mohamed kutokana na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa Mkanyageni (CUF),
Habibu Mnyaa aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge lilipokaa kama
kamati ya kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15.
Mnyaa alisema Wizara ya Katiba na Sheria ni muhimu lakini imekuwa
ndiyo ya kwanza kuvunja sheria na haki za binadamu na akataka ufafanuzi.
Hata hivyo, aliposimama kujibu swali hilo, Jaji Werema alimwambia
Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar na siyo katika Bunge la
Jamhuri kwa kuwa si kila kitu kitaulizwa ndani ya Bunge hilo.
“Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake,
namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna
majibu,” alisema Werema.
Mara baada ya Bunge kurejea, Mbarouk aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa kauli hiyo kwamba ilikuwa ya kibaguzi.
“Mheshimiwa Spika, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Alisema ubaguzi huo umewabagua wabunge ambao wamekula kiapo cha
kulitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano na unaonyesha namna ambavyo
Wazanzibari wanabaguliwa.
“Mheshimiwa Spika, yanapofanyika
mambo kama hayo na wewe mwenyewe uko hapa unaona ni sawa na kubariki
jambo hilo, huu ni ubaguzi unaoufanya wewe kwa kuwa lilifanyika ukiona
bila hata ya kukemea,” alisema Mbarouk.
Hata hivyo, Spika alipinga na kusema: “Hakuna mwongozo wowote
kwa kuwa hata wewe umevunja sheria kwani hata nilipokuambia kaa chini
umeendelea kuzungumza, tunaendelea…. Katibu (akimtaka Katibu wa Bunge
kutoa mwelekeo wa shughuli iliyokuwa inafuata ambayo ilikuwa Hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).”
Baada ya kauli ya Spika, wabunge wa Zanzibar walihamasishana na
kuamua kutoka nje kwa wakati mmoja na huku wenzao wa upinzani
wakiendelea kutafakari cha kufanya. Wakati huo, Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mathias Chikawe alikuwa akisoma hotuba yake.
Home
»
»Unlabelled
» Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema Alikoroga Bungeni.
Topics:
About Unknown
Kwa jina Naitwa MWEUSI waweza wasiliana nami namba 0757420837, 0629208856 au email: timotheosodoka@gmail.com
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni: