Askari
Polisi aliyefukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu mwaka 2012 baada ya
kukutwa na silaha katika ukumbi wa disko mkoani Kilimanjaro, James Marwa
(26) amekamatwa na Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime-Rorya akidaiwa
kuwa katika harakati za kwenda kufanya uhalifu eneo la mgodi wa
Nyamongo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime-Rorya, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kukamatwa kwa Marwa.
Mambosasa
alisema kwa sasa anashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya
riffle ikiwa na risasi tano ya kampuni ya ulinzi ya Paroma Security na
kukiri kwamba alikuwa anaenda kuungana na wenzake kwenda kufanya uhalifu
mgodi wa Nyamongo.
Akifafanua
Kamanda Mambosasa alisema Julai 29 walipata taarifa kutoka kwa raia
wema kuonekana mtuhumiwa maeneo ya Mtaa wa Magamaga, kata ya Sabasaba,
Tarime, akiwa na bunduki aina ya riffle yenye namba 58368 TZCAR 5963
ikiwa na risasi tano.
“Tulifuatilia na kumkamata mtuhumiwa akiwa na silaha
hiyo, tumemhoji na kubaini kuwa kwa hivi sasa alikuwa akifanya kazi ya
ulinzi katika kampuni ya ulinzi ya Paroma Security eneo la ujenzi wa
Mizani huko Sirari na alipohojiwa zaidi alidai alikuwa akienda Nyamongo
mgodini kuungana na wenzake kufanya Uhalifu,” alisema Kamanda.
. Alisema watamfikisha mtuhumiwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
_POLISI ALIYEFUKUZWA KAZI AKAMATWA AKIJIANDAA KUFANYA UHALIFU

Hakuna maoni: