JESHI
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, jana imelitolea ufafanuzi
sakata la kukamatwa kwa askari ‘feki’ wa Kikosi cha Usalama Barabarani
(trafiki), katika kata ya Chamazi, Mbagala Majimatitu, Wilaya ya Temeke,
jijini humo.
Mtuhumiwa huyo, Bw. Robson Emmanuel (30), alikamatwa Agosti 2 mwaka huu, akijifanya Ofisa wa Polisi katika kikosi hicho.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa kanda hiyo,
Kamishna Suleiman Kova, alisema mtuhumiwa aliwahi kuwa mwajiriwa wa
jeshi hilo kuanzia mwaka 2000 akiwa na namba F2460 lakini alifukuzwa
kazi kwa fedheha Machi 3 mwaka 2014, Kibaha, mkoani Pwani akiwa na cheo
cha Stesheni Sajenti.
“Katika
uchunguzi wetu, tumebaini mtuhumiwa alikuwa akijitambulisha kama
askari, hivyo alifanikiwa kuwatapeli wananchi wengi na kujipatia kiasi
kikubwa cha fedha kwa njia za udanganyifu,” alisema.
Aliongeza
kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa amevaa sare za jeshi hilo na cheo
cha Stesheni Sajenti pia alikutwa na gari aina ya Cresta namba T 723
BAK yenye rangi nyeupe ambayo alilitumia kuzunguka maeneo mbalimbali ya
jiji hilo na kutapeli.
“Katika
gari hilo, polisi walipekua na kukuta radio call moja yenye namba GP380
aina ya Motorola, leseni za udereva 40, stakabadhi mbili za Serikali
zenye namba A0531562 na A1672464, police loss report mbalimbali, kofia,
beji, ratiba ya mabasi yaendayo mikoani na vitu vingine mali ya Jeshi la
Polisi.
“Pia
mtuhumiwa alipekuliwa nyumbani kwake ambapo polisi walikuta sare za
jeshi hilo rangi ya kaki pea nne, pea tatu ambazo ni sare za Kikosi cha
Usalama Barabarani, koti moja la mvua la kikosi hicho, reflector 8 za
kuongozea magari, kofia, mikanda ya jeshi na vyeo vitatu vya Stesheni
Sajenti,” alisema Kamishna Kova.
Katika
hatua nyingine, Kamishna Kova alisema jeshi hilo linawashikilia
majambazi wawili kwa tuhuma za kujihusisha na unyang’anyi wa kutumia
silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Julai 30 mwaka huu, eneo la Makumbusho Kijitonyama kutokana na msako mkali wa jeshi hilo.
“Watuhumiwa
hawa baada ya kupekuliwa majumbani mwao, walikamatwa na bastola mbili,
moja aina ya Grock 17 yenye namba B019259 iliyotengenezwa nchini Czech
ikiwa na risasi 13 ndani ya magazine, nyingine aina ya Chinese
iliyofutwa namba zake ikiwa na risasi moja ndani ya magazine,” alisema.
Aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni Fredy Steven (25), ambaye ni mfanyabiashara,
mkazi wa Kiwalani na Irene Nyange (36), mfanyabiashara na mkazi wa
Kijitonyama ambapo uchunguzi unakamilishwa ili watuhumiwa waweze
kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Hakuna maoni: