Hapa ni katika Msikiti wa Masjid Latif
Ahmadiyya Muslim Jamaat Nsalala uliopo kijiji cha Nsalala ,kata ya Tinde
wilaya ya Shinyanga ambapo leo Jumapili Mei 22,2016 Jumuiya ya Waislam
wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga (Ahmadiyya Muslim Jamaat Shinyanga)
imefanya mkutano wa Mwaka wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Shinyanga ukiwa na
kauli mbiu ya " Love For All Hatred For None (Mapenzi Kwa Wote Bila
Chuki Kwa Yeyote".
Mgeni rasmi alikuwa katibu tawala
msaidizi idara ya uchumi na uzalishaji mkoa wa Shinyanga Mohammed Idd
Nchira aliyemwakilisha kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga John Mongella
huku waumini wa dini hiyo kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga
wakihudhuria mkutano huo.
Mkutano huo uliolenga kuhamasisha amani
katika jamii kwa kuwakumbusha waumini kumjua mwenyezi mungu hali
itakayosaidia kupunguza hata kumaliza kabisa vitendo vya kihalifu
ikiwemo mauaji ya watu wasio na hatia kama vile vikongwe na albino,
umehudhuriwa pia na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry (pichani juu).
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa
Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood
Chaudhry alieleza kusikitishwa na kitendo cha mauaji ya watu watu
msikitini na kuongeza kuwa dini ya kiislam hairuhusu vitendo kama hivyo
huku akiviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kubaini wahusika wa
kitendo hicho haramu.
Kupitia mkutano huo jamii imeelimishwa
juu ya dhana potofu dhidi ya uislamu ambapo baadhi ya watu wamekuwa
wakihusisha dini hiyo pamoja na vikundi vya kigaidi mfano wa Boko haram,
Isis, Al-shabaab na vingine vingi ambavyo vimekuwa vikidhuru binadamu.
Mada mbalimbali zimetolewa na viongozi
wa jumuiya hiyo ikiwemo nafasi ya dini katika maisha ya binadamu,malezi
ya watoto na majukumu ya wazazi sawa na mafundisho ya dini ya
kiislamu,umuhimu wa kuwa kiongozi (Khalifa) wa kiroho na barakaza
ukhalifa pamoja na masharti ya kujiunga na jumuiya hiyo(masharti 10 ya
Baiat na wajibu wa waumini.
Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde alikuwepo wakati wa mkutano huo,ametusogezea picha 55 kilichojiri..
Hapa ndipo Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya
Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga waumini wa dini ya kiislamu
kutoka Jumuiya hiyo kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga
wamejitokeza kwa wingi kusikiliza mawaidha mbalimbali kutoka kwa
viongozi wa Jumuiya hiyo pamoja na wageni waalikwa akiwemo kaimu mkuu wa
mkoa wa Shinyanga Mohammed Idd Nchira
Bango likionesha kilichokuwa kinaendelea
Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya
Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania Abdulrahman Mohammed Ame akitoa
mada kuhusu Haja ya nafasi ya dini katika maisha ya binadamu ambapo
alitumia fursa hiyo kuitaka jamii kutenda mambo mema na kujiepusha na
vitendo vya kihalifu ikiwemo kuua watu wenye ulemavu wa ngozi na
vikongwe.
Alisisitiza kuwa uislamu ni dini ya
amani hivyo kuwataka binadamu kuishi kwa amani na kwamba kitendo cha
kuua mtu mmoja ni sawa na kuua dunia nzima.Hata Hivyo Ame alisema sera
ya jumuiya hiyo ni kutochanganya siasa na dini
Meza kuu,wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa
Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood
Chaudhry,kushoto kwake ni mgeni rasmi Mohammed Idd Nchira,akifuatiwa na
rais wa Jumuiya hiyo Kanda ya Ziwa Salim Thani,wa kwanza kushoto ni
Naibu rais wa jumuiya hiyo Kanda ya ziwa Yahaya Kamba Ulaya.Wa kwanza
kulia ni Mbashiri wa kanda ya ziwa wa jumuiya hiyo Sheikh Waseem Khan
Waumini wa dini ya Kiislam kutoka maeneo ya mjini na Vijijini ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga waliojitokeza katika mkutano huo
Mgeni rasmi katika mkutano huo Mohammed Idd Nchira akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Moja ya mabango yaliyokuwa katika mkutano huo
Mgeni rasmi katika mkutano huo Mohammed
Idd Nchira akiwahutubia waumini wa dini ya kiislamu wa Jumuiya ya
Waislam wa Ahmadiyya ambapo alisema suala amani katika jamii ni watu
wote hivyo kuwataka watanzania kudumisha amani ya nchi kwa kuepuka
kutenda uhalifu
Aliyesimama ni Afisa wa polisi kutoka
ofisi ya mkuu wa upepelezi na makosa ya jinai mkoa wa Shinyanga Issa
Ramadhan akitoa neno ambapo alisema jamii yenye malezi mema haiwezi kuwa
na vitendo vya kihalifu na kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na
jeshi la polisi kuwafichua watu wote wanaofanya vitendo vya uhalifu
Wanawake wa Kiislam wakiwa katika
Msikiti wa Masjid Latif Ahmadiyya Muslim Jamaat Nsalala uliopo kijiji
cha Nsalala ,kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga wakifuatilia kilichokuwa
kinaendelea katika mkutano huo wa mwaka,ambapo kwa mara ya pili sasa
mkutano kama huo unafanyika mkoani Shinyanga,mkutano mwingine ulifanyika
mwaka 2014
Wanawake wakiwa msikitini
Mkuu wa kituo cha polisi Tinde Mkaguzi
Msaidizi wa polisi Wilbert Sichone aliyemwakilisha mkuu wa polisi wilaya
ya Shinyanga,akitoa neno katika mkutano huo ambapo aliwaomba viongozi
wa dini mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya dini kwani vitendo vingi vya
kihalifu vimekuwa vikijitokeza kutokana na jamii kutokuwa na hofu
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nsalala
kilichopo katika kata ya Tinde Sandeko Machongo akitoa shukrani kwa
jumuiya hiyo kwa kushirikiana na wananchiwa kijiji hicho katika masuala
mbalimbali ikiwemo ujenzi wa visima vitatu vya maji
Waumini wakifutilia kilichokuwa kinaendelea kwenye mkutano huo
Mbashiri/Sheikh wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya mkoa wa Morogoro Asif Butt akitoa mada ya Masharti kumi ya
Baiat na wajibu wa waumini wa jumuiya hiyo.Miongoni mwa masharti hayo ni
pamojana waumini kutojihusha na vitendo vya kishirikina akieleza kuwa
ushirikina ndiyo chachu ya maovu/mabaya yote katika jamii
Tunamsikiliza Mbashiri wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya mkoa wa Morogoro Asif Butt
Mbashiri wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya mkoa wa Morogoro Asif Butt alitumia fursa hiyo kuwataka
wanadamu kuwapuuza baadhi ya watu wanaodai kuwa jumuiya hiyo haifuati
misingi ya dini ya kiislam huku akiongeza kuwa tofauti yao na wengine
wao wanafanya misingi ya dini kwa vitendo badala ya maneno
Meza kuu wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo
Tunafuatilia kinachoendelea hapa......
Waumini wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo
Watoto wakiwa msikitini wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea katika mkutano huo
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry akitoa hotuba yake ambapo
pamoja na mambo mengine alisema jumuiya hiyo ambayo ipo katika nchi 207
duniani kila siku imekuwa ikiwakumbusha waumini kuishi katika misingi
ya kumfuata mwenyezi mungu,kwasisitiza waumini kushika mafundisho kwa
vitendo badala ya maneno ili wawe raia wema ili jamii iishi kwa amani
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry alieleza kusikitishwa na
mauaji ya watu watatu jijini Mwanza katika msikiti na kusema kuwa dini
ya kiislamu hairuhusu watu kuuana na kuwaomba wakazi wa Mwanza na nchi
kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya ulinzi na usalama
vikifanya uchunguzi ili kujua chanzo cha mauaji na kuwabaini wahusika wa
mauaji hao
Mkutano unaendelea
Mkutano unaendelea
Tunamsikiliza Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry akisisitiza kuwa jumuiya
hiyo ya kimataifa ina uongozi wake na inaendeshwa kwa heshima kubwa na
siku zote wamekuwa wakihubiri amani
Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry akiwaomba watanzania
kuachana na vitendo vya kihalifu ikiwemo kuua albino na vikongwe kwa
imani za kishirikina
Kulia ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya
ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania Abdulrahman Mohammed Ame
akitafsiri hotuba ya Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania
Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry aliyokuwa anaitoa kwa lugha ya
Kiingereza
Kulia ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya
ya Waislam wa Ahmadiyya nchini Tanzania Abdulrahman Mohammed Ame
akitafsiri hotuba ya Mkuu wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania
Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry aliyokuwa anaitoa kwa lugha ya
Kiingereza.Chaudhry alisema ili jamii iishi kwa amani ni vyema binadamu
wakaishi kwa kupendana na kuacha vitendo vya kishirikina na kulipishana
visasi
Mabango yakiwa katika eneo la mkutano
Mabango yakiwa na ujumbe wa aina mbalimbali katika eneo la mkutano
Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya ina
kiongozi mkuu duniani ambaye sasa anaitwa Khalifatul Masih v Hazrat
Mirza Masroor Ahmad ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kujitahidi
kuwaomba wanadamu kuishi kwa kuzingatia misingi ya amani.
Viongozi wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya wakijiandaa kuomba dua wakati wa mkutano,kushoto ni Mkuu wa
Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood
Chaudhry katikati ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya nchini Tanzania,kulia ni rais wa Jumuiya hiyo Kanda ya Ziwa
Salim Thani
Kulia ni rais wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya Kanda ya Ziwa Salim Thani akiteta jambo na kiongozi wa Jumuiya
ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga Shaaban Luseza (kushoto)
Kulia ni rais wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya Kanda ya Ziwa Salim Thani akiteta jambo na kiongozi wa Jumuiya
ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga Shaaban Luseza (kushoto)
Waumini wa Jumuiya hiyo wakiwa wamesimama wakati wa kuomba dua
Waumini wakiwa tayari kuomba dua
Waumini wakiwa wamesimama wakati wa kuomba dua
Tunaomba dua
Akina mama wakiwa ndani ya msikiti wakiomba dua
Viongozi wa Jumuiya ya Waislam wa
Ahmadiyya wakiomba dua wakati wa mkutano,kushoto ni Mkuu wa Jumuiya ya
Waislam wa Ahmadiyya Tanzania Maulana Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry
katikati ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya
nchini Tanzania,kulia ni rais wa Jumuiya hiyo Kanda ya Ziwa Salim Thani
Kushoto ni Yusuph Mgeleka kutoka mkoa wa
Shinyanga ,Mubarak Nyamihasi kutoka mkoani Mwanza(katikati) na Mussa
Kaswezi kutoka mkoa wa Kagera(kulia) wakiimba shairi la kuagana wakati
wa kufunga mkutano huo
Wanawake na watoto wakiwa nje ya msikiti baada ya mkutano kufungwa
Bango katika mkutano huo
Picha ya kumbukumbu baada ya mkutano huo kumalizika
Bango likiwa katika mkutano huo
Bango likiwa katika mkutano huo wa mkoa wa Shinyanga ulioandaliwa na Jumuiya ya Waislam wa Ahmadiyya Mkoa wa Shinyanga
Bango likionesha ujumbe mzuri
Bango jingine lilokuwa katika mkutano huo
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
hotuba ya mheshimiwa
mkuu wa mkoa wa shinyanga
Katika
mkutano wa mwaka wa jumuiya ya waislamu waahmadiyya kanda ya mwanza, shinyanga
na simiyu
tarehe 22
mei 2016
Mheshimiwa Amir na Mbashiri Mkuu wa
Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya
Tanzania,
Sheikh Tahir Mahmood,
Viongozi wa Kamati kuu ya Jumuiya ya
Waislamu Waahmadiyya nchini
Viongozi waalikwa wa ngazi
mbalimbali
Mabibi na Mabwana;
Assalaam Alaikum, (Amani iwe juu
yenu).
Awali ya yote, natoa shukurani zangu
za dhati kwa kunikaribisha katika mkutano huu wa Jumuiya yenu ya Ahmadiyya hapa
katika Kanda ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu.
Nimefahamishwa kuwa wageni mbalimbali kutoka mikoa ya kanda
hii wakiwemo viongozi wa kijamii na kisiasa wamealikwa katika mkutano huu.
Mheshimiwa Amir,
Nimefahamishwa pia kwamba Jumuiya
yenu ya Ahmadiyya imekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 80 sasa na kwamba
katika muda huo wote imeonyesha mfano mzuri wa upendo na kuvumiliana na waumini
wa itikadi zingine hapa nchini. Hali hiyo ni licha ya kuwa baadhi ya waumini wa
madhehebu mengine wanaziona itikadi zenu zinatofautiana kidogo na za kwao na
wakati mwingine kukubezeni. Hata hivyo mmekuwa mkihubiri kwa subira, upendo na uvumilivu
huku mkizingatia ule usemi wenu maarufu wa “Love For All Hatred for None”
yaani “Upendo kwa wote bila chuki kwa yeyote”
Swala la kuishi kwa kuvumiliana na
kuheshimiana miongoni mwa wanadini na waumini wa imani mbalimbali sio tu kwamba
ni la muhimu bali ni la lazima katika nchi kama yetu na ulimwengu wa leo wa
utandawazi kwa ujumla, kwani kwa bahati mbaya kwa kadri dunia inavyosonga mbele
tunakabiliwa na tatizo kubwa la watu wenye misimamo mikali ya itikadi za kidini
isiyokubali kuvumilia na kuheshimu imani wa wengine, tatizo ambalo ni miongoni
mwa vyanzo vikubwa vya uvunjifu wa amani duniani leo.
Aidha nimepata kufahamishwa kwamba
sera ya Jumuiya yenu kama Jumuiya ya kidini duniani kote ni kutokujiingiza
katika masuala ya kisiasa ya nchi yoyote, isipokuwa waumini wenu wanaweza
kushiriki katika siasa za nchi zao katika ngazi ya mtu binafsi. Sera yenu hii ya
kushughulikia masuala ya dini bila kuchanganya na siasa ni sera muhimu kwani
ndiyo inayoweza kuhakikisha kwamba waumini wenu hawagawanyiki kwa misingi ya
vyama vya siasa bali daima wanabaki kuwa kitu kimoja; Na jambo hilio nalo ni
muhimu kwa ajili ya mandeleo ya Jumuiya husika na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Ninakupongezeni kwa msimamo huu na ninawaomba muendelee hivyo.
Mheshimiwa Amir,
Bila shaka nyote mnafahamu ya kuwa
Serikali ya Tanzania haina dini, bali Watanzania ndio wenye imani mbalimbali za
dini. Serikali ina wajibu wa kuziheshimu dini hizo kwa mujibu wa katiba ya nchi,
na tunaamini kwamba jambo hili la kutoa uhuru wa dini/kuabudu limechangia sana katika
amani ya nchi yetu. Mnajua kwamba ziko nchi duniani, dini fulani huonekana kuwa
ndiyo dini ya taifa na kupewa haki zote na kuwaacha wenye imani zingine wakati
mwingine wakiitwa ‘minorities’ wakinyimwa haki yao ya msingi ya kuamini na
kuabudu sawa na uelewa wao. Ninakuhakikishieni kwmaba Serikali yenu Ya Tanzania
itabaki na msimamo huu daima wa kuhakikisha kwamba kila mtanzania yuko huru
kuamini na kuabudi jinsi apendavyo maadamu tu havunji sheria za nchi wala
kusababisha shida kwa wengine.
Aidha Serikali inatambua mchango
mkubwa ambao Jumuiya za kidini hutoa kwa jamii, mathalan huduma za maji, elimu,
matibabu n.k. Jumuiya yenu haipo nyuma katika suala hili. Nimefahamishwa kwamba
kwa takriban miaka mitatu sasa kupitia mradi wa “Water for Life” mumekuwa mkiendelea na
uchimbaji na ukarabati wa visima vya maji safi katika maeneo ya Dar es Salaam, Pwani,
Morogoro Dodoma na kwingineko.
Nimefurahishwa sana kusikia kwamba mnaendelea
na ujenzi wa miskiti katika maeneo kadhaa ya vijiji vya Mkoa wetu wa Shinyanga
na kwamba mwaka huu mnao mpango wa kuchimba visima vipatavyo 30 katika vijiji
hivyo. Jambo hili litaongeza kasi ya maendeleo ya kielimu na kijamii katika
vijiji hivi.
Mheshimiwa Amir,
Sisi tukiwa viongozi wa Serikali
tunaelewa kwamba dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya ustaarabu
wa mwanadamu kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya waumini
waepukane na maovu mbalimbali mathalan utumiaji wa madawa ya kulevya, wizi,
rushwa, uzinzi (ambao hupelekea madhara mengi yakiwemo ugonjwa wa Ukimwi), uzururaji n.k. Bali dini hasa zinatufundisha
kumuamini Mungu na kujiepusha na matendo ya ushirikina. Aidha kwa kuepuka tabia
hizo mbaya jamii husonga mbele haraka kwenye maendeleo ya kiuchumi. Kwa ujumla
iwapo dini zetu zitatumika vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza agizo la
Mheshimiwa Rais wetu la 'Hapa kazi tu' kwani kila mtu ataepuka uzembe na
kuwajibika ipasavyo.
Hivyo ni imani yangu kwamba Jumuiya
yenu kama zilivyo taasisi zingine za kidini mnaendeleza kazi kubwa ya kupambana
na maovu katika jamii yetu kwa kuwapatia waumini wenu na wananchi kwa ujumla
elimu na maarifa ya kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho. Hapa kwenye
mikoa yetu ya kanda hii kuna haja kubwa sana ya wananchi kupata elimu sahihi ya
maadili kwani kuna matendo mengi yasiyo mazuri hasa ya ushirikina na mauwaji
dhidi ya vikongwe.
Napenda niwahakikishieni kuwa
Serikali inaunga mkono juhudi za Jumuiya yenu an Jumuiya zingine za kidini katika kupiga vita maovu ya kila
aina.
Kama mnavyoelewa moja ya kipaumbele
kikubwa cha Serikali yetu ni kupambana na ufisadi uliozagaa katika maisha yetu.
Ufisadi huu ni kiashiria tosha cha hali yetu ya kimaadili ilivyo mbaya. Jumuiya
na taasisi za kidini zinaweza kusaidia sana katika jambo hili iwapo zitaamua
kupambana na ufisadi kutoka ndani mwao kwa kuwafahamisha waumini wao juu ya
ubaya wa tabia hiyo chafu ambayo inapingwa na mfundisho ya dini zote.
Sawa na uelewa wangu hakuna dini
ambayo inafundisha ufisadi, wizi, chuki, uhasama, dhuluma, uonevu na fujo, bali
dini zote kwa njia moja au nyingine zinafundisha huruma, upendo, haki, uadilifu
na kutendeana kwa wema kama ndugu.
Hivyo sote kwa pamoja tuhubiri
maadili haya ili tuweze kujenga jamii ya Watanzania yenye kupendana,
kuhurumiana, kuheshimiana na kusaidiana.
Mheshimiwa Amir na waumini wote
Mwisho; baada ya kusema hayo naomba
tena niwashukuruni kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika mkutano wenu huu
na ninawatakia heri na mafanikio. Yale yote mtakayokumbushana muweze
kuyatekeleza.
Wasslaam.
Hakuna maoni: