SHIRIKISHO
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limewashtaki kwa Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, baadhi ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na
wakurugenzi wa halmashauri na manispaa, wanaowaweka ndani na kuwashusha
vyeo watumishi wa umma bila sababu za msingi.
Malalamiko
hayo yalitolewa jana mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus
Mgaya, alipokuwa akisoma risala katika mkutano mkuu wa sita wa
shirikisho hilo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa.
Pamoja
na Majaliwa, walikuwapo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angelah
Kairuki.
Katika
maelezo yake, Mgaya alilalamikia tabia ya viongozi hao na kusema
inakatisha tamaa watumishi wa umma kwa kuwa wanafanya kazi kwa hofu.
Kwa
mujibu wa Mgaya, utaratibu huo hawakubaliani nao kwa kuwa umekuwa
ukifanywa bila ya kufuata kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Sisi
kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi, hatukubali jinsi viongozi hao
pamoja na wanasiasa wengine, wanavyowafukuza kazi watumishi kwa kutaka
mambo yao yaende vizuri.
“Tungependa
kuona sheria zinafuatwa pale ambapo masuala ya nidhamu ya mfanyakazi
yanahusika ili kuondoa maonevu yasiyokuwa ya lazima, kwani hata
waswahili husema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni,’’ alisema
Mgaya huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.
Akijibu
malalamiko hayo, Majaliwa alisema Serikali ya Rais Dk. John Magufuli
itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora, ili
kuhakikisha haki za wafanyakazi nchini zinalindwa ipasavyo.
Kutokana
na hali hiyo, aliwaagiza viongozi wa kisiasa nchini walioko katika
wizara mbalimbali, mikoani, wilayani, idara za Serikali, halmashauri na
taasisi zote za Serikali, wazingatie utawala wa sheria kushughulikia
masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi.
“Pamoja na hayo, lazima wafanyakazi wote nchini mtekeleze majukumu yenu kwa nidhamu, muwajibike na muwe waadilifu pia.
“Ni
wazi kwamba nidhamu ya kazi imeporomoka kidogo kutokana na watumishi
kutotimiza wajibu wao na wengine ni wabadhilifu wa mali za umma.
“Hao
Serikali haitawafumbia macho, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa
mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,’’ alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kuhusu
mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, aliwaagiza waajiri wote nchini,
kutoa mikataba hiyo haraka iwezekanavyo kwa wafanyakazi wao.
Pia,
aliwaagiza maofisa wa kazi nchini, kuhakikisha kila mwajiri anafikiwa
na watakaokutwa wakikiuka taratibu za ajira, wachukuliwe hatua za
kinidhamu.
Chanzo-Mtanzania
Hakuna maoni: