Najua hakuna aliyetarajia kuona hili likitokea lakini kwa uwezo wa Mungu limefikia mwisho.
Nakumbuka Machi 21 ya mwaka huu kaka yangu Fredrick Bundala aliandika
makala iliyokuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “Ninachotamani: Lady
Jaydee na Clouds Media Group wamalize tofauti zao” hatimaye hilo
limesikika na kila kitu kimeonekana kuwa sawa kutokana na pande zote
mbili kuamua kufukia mabaya yote yale yaliyowahi kutokea.
Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, napenda kumpongeza Mkurugenzi
wa Vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kwa busara yake
aliyoitumia ya kujibu swali aliloulizwa kwenye kipindi cha XXL kuhusu
kumaliza ugomvi wao na malkia wa muziki wa Bongo Fleva, Jaydee.
“Tatizo ni kwamba hakuna ambacho hatujamaliza, tulimaliza, tunasubiri
order. Unajua kimsingi ulipopewa order ya kwamba ‘nyimbo zangu usipige,
jina langu usiseme kwenye chombo chako, vyovyote itakavyokuwa mimi
sitaki kusikia hiyo kitu’ hiyo ndio order. Kwahiyo labda tukikutana,
nimuombe tena [Lady Jaydee] kama tutaruhusiwa kufanya hiyo kitu,”
alisema Ruge kwenye kipindi hicho.
Aliongeza kwa kusema kuwa ni muda mrefu hajawahi kukutana na Lady
Jaydee, japo alidai ‘hata leo nikipata nafasi ya kahawa nitashukuru sana
kwa huo mwaliko.’
Hatimaye ujumbe ule ulimfikia Jaydee na nampongeza hakutaka kuliacha
jambo hilo lipite kwa kuwa limedumu kwa muda mrefu na hakuna jipya
lililotokea kwa kuwa kila mtu bado anafanya kazi zake huku mashabiki
ndio wakibaki njia panda wakishindwa cha kufanya.
Jumatano hii uongozi wa Jide ulitoa taarifa yake rasmi kuwa wapo tayari
kufanya kazi tena na kituo hicho cha redio. “Hatuna tatizo na Clouds
Media Group kuanza kupiga nyimbo za Lady Jaydee. Wanaweza kuanza kupiga
wakati wowote watakapokuwa tayari kwakuwa chochote kilichotokea hapo
nyuma kimefikia tamati, la msingi sasa ni amani na upendo vitawale.
Kuanzia leo wana uhuru wa kupiga na kutaja jina la Lady Jaydee kadri
wawezavyo,” yalisema maelezo yake.
Kitendo hicho kilichofanywa na pande zote mbili kitawarudisha upya tena
baadhi ya mashabiki waliogawana upande pamoja na kuwapa nafasi wasanii
ambao walikuwa wakitamani kufanya kazi na Jide kwa muda mrefu lakini
walikuwa wakihofia nyimbo zao kutochezwa kwenye kituo hicho.
Kama hili limewezekana basi natamani pia kuona siku moja wasanii wengine
ambao hawapatani na kituo hicho na vituo vingine vya habari
wakiyamaliza matatizo yao na kuendelea kuufanya muziki wetu kusonga
mbele kwa kuwa wote tupo kwenye safari moja na kila mtu anamtegemea
mwenzake ili kuhakikisha hilo linatimia.
By Salum Kaorata
Topics: habari
About Unknown
Kwa jina Naitwa MWEUSI waweza wasiliana nami namba 0757420837, 0629208856 au email: timotheosodoka@gmail.com
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni: