Kamanda wa jeshi jeshi la polisi mkoa wa
Shinyanga ACP Muliro Jumanne akionesha vifaa vya uganga vya waganga wa
kienyeji 22 waliokamatwa wakidaiwa kujihusisha na upigaji ramli
chonganishi hivi karibuni-Picha kutoka maktaba ya Malunde1 blog
Wananchi wenye hasira kali wamemuua mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa
jina la Kashinje Kashinje(55), mkazi wa kijiji cha Singita kata ya
Usanda wilayani Shinyanga kwa kumshambulia kwa silaha za jadi wakati
akijaribu kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 20 (jina linahifadhiwa)
aliyefika nyumbani kwa mganga huyo kupata tiba ili apate mtoto.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne
Muliro tukio hilo limetokea Novemba 29 mwaka huu majira ya saa tano
asubuhi.
Kamanda Muliro alisema mganga wa kienyeji Kashinje Kashinje alifariki
dunia alipokuwa njiani akipelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa kwa kitu
chenye ncha kali jicho la kulia ma kupigwa kwa fimbo mgongoni na watu
waliojichukulia sheria mkononi.
“Watu hao walijichukulia sheria mkononi baada mganga huyo kujaribu
kumbaka mwanamke (jina linahifadhiwa) mkazi wa kijiji cha Ishinabulandi
wilaya ya Shinyanga ambaye alikuwa akimtibu kwa tiba za asili ili aweze
kupata mtoto”,alieleza kamanda Muliro.
Alisema tatizo lililompeleka mwanamke huyo kwa mganga ni kupata tiba ili aweze kupata mtoto.
Kamanda Muliro alibainisha kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa za
kimwili na uongo wa kimatibabu wa kutaka kumuingilia kimwili mgonjwa
wake baada ya kumlewesha kwa dawa za kienyeji.
Aliongeza kuwa kutokana na kitendo hicho cha mganga wa kienyeji,mwanamke
huyo alipiga kelele za kuomba msaada ndipo wananchi walifika na kuanza
kumshambulia mganga huyo na kumsababishia maumivu makali yalisababisha
chanzo cha kifo chake.
Kamanda Muliro alisema watu wawili wanaohojiwa kuhusiana na tukio hilo ambao ni Masaganya Katambi (45) na Shija Sele (40).
Hakuna maoni: