NA SAMSON CHACHA,Gazeti la Uhuru, TARIME
MKAZI wa Kijiji cha Nyamwaga wilayani hapa mkoani Mara, Mbusiro Muyuyi, ameuawa kwa kukatwakatwa kwa panga kichwani na shemeji yake.
Mauaji hayo yaliyowashitua wengi wilayani hapa, chanzo chake ni
mbwa wa mtuhumiwa, Mwita Muyuyi (17), kula mayai ya kuku wa marehemu.
Habari za kuaminika zimesema kuwa, Mbusiro (45), alimtuhumu shemeji
yake kuwa, mbwa wake amekula mayai ya kuku, hali iliyoibua mzozo mkubwa
baina yao.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/ Rorya, Justus
Kamugisha, alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika kitongoji
cha Ntarachagine.
Alisema wakati mzozo huo ukiendelea, Muyuyi alikuwa ameshika panga
na ghafla alianza kumshambulia mke wa kaka yake sehemu mbalimbali za
mwili wake.
Kamanda Kamugisha alisema baada ya tukio hilo, Mbusiro alikimbizwa
hospitali kwa matibabu, lakini akiwa kwenye zahanati ya Nyarero, hali
yake ilizidi kuwa mbaya na kufariki dunia.
Tayari mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kabla
ya kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.
Kamanda Kamugisha alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha
tabia za kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafikishe migogoro
kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zaidi.
Hakuna maoni: