Siku
chache baada ya kutwaa Taji la Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Zuberi
Mtemvu ameibua mshangao wa aina yake kutokana na utata wa umri wake.
Utata
huo uliibuka saa chache mara baada ya shindano hilo kufanyika Oktoba
10, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam ambapo
wadau mbalimbali walianza kuhoji.
UTATA WENYEWE HUU HAPA
Mara
baada ya mrembo kutangazwa mshindi, habari za chini kwa chini zilidai
kwamba Sitti alijinasibu kuwa ana umri wa miaka 18 na elimu ya (digrii
mbili) (masters), mambo ambayo yaliwashtua wengi na kuanza kuhoji
uhalali wa umri huo ukilinganisha na kiwango chake cha elimu.
“Mh!
Haiwezekani, kama ana miaka kumi na nane atakuwa alianza darasa la
kwanza akiwa na miaka miwili?” Alihoji mdau mmoja ambaye hakupenda jina
lake litajwe.
ELIMU YA BONGO IKOJE?
Kwa
mfumo wa elimu nchini ulivyo, mtoto huanza darasa la kwanza akiwa na
kati ya miaka mitano hadi saba, jambo ambalo haliingii akilini kwa Sitti
kwani hesabu zinakataa hata kwa mtu asiyesomea mahesabu.
Ukiachilia
mbali shule ya awali (nursery) ambayo huchukua kati ya miaka miwili
hadi mitatu, ukihesabu miaka saba ya elimu ya msingi (primary), miaka
minne ya sekondari (ordinary level), miaka miwili ya kidato cha tano na
sita (advanced level) na miaka mitatu ya shahada kwanza (bachelor
degree), jumla ni miaka 16.
Pia
kuna madai kwamba ametumia mwaka mmoja kusomea shahada ya pili
(masters) huku kukiwa na muda ambao kwa kawaida huwa unapotea baada ya
kumaliza kidato cha nne kwenda cha tano na baada ya kumaliza kidato cha
sita kwenda chuo kikuu.
INA MAANA ALIANZA DARASA LA KWANZA AKIWA NA MIAKA MIWILI?
Kwa
mantiki hiyo, kama kweli Sitti ana umri wa miaka 18, basi atakuwa
alianza darasa la kwanza akiwa na miaka miwili, jambo ambalo ni msamiati
mpya kwa jamii ya Kibongo.
BABA MZAZI ANASEMAJE?
Ili
kuondoa utata na tafrani inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii hadi
kufikia hatua ya watu kutukanana, mwandishi wa habari hizi alimtafuta
baba mzazi wa Sitti ambaye ni Mbunge wa Temeke, Dar kwa leseni ya Chama
cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Abbas Zuberi Mtemvu alipopatikana alifunguka:
“Umri
wake ni kama alivyosema mwenyewe siku ile (miaka 18), kama mnataka
kujiridhisha nendeni hata huko Miss Tanzania mtaoneshwa passport (hati
ya kusafiria) yake…,” alisema mzazi huyo huku akiomba aachwe kwanza ashughulikie wananchi wa jimboni kwake.
TUMUAMINI MZAZI?
Hata
kama tukiamini maelezo ya mzazi, maana yake ni kwamba mrembo huyo
alianza darasa la kwanza akiwa na miaka miwili, jambo ambalo linazidi
kuongeza utata katika sakata hilo.
AKATAA KUHITIMU MASTERS
Alipobanwa
zaidi kuhusu taarifa zinazosema kuwa mwanaye amehitimu masters, mzazi
huyo alikanusha na kudai kwamba mwanaye amehitimu bachelor degree
(shahada).
“Kuhusu
masters mnakosea, mwanangu hana masters, ana bachelor, nilimshauri
achukue masters lakini akaomba nimuache ashiriki kwanza mashindano ya
u-miss ndiyo aje aendelee baadaye,” alisema mheshimiwa huyo.
NI AIBU NYINGINE KWA LUNDENGA?
Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, suala la warembo kudanganya
umri limekuwa ni sugu hivyo kuleta tafsiri ya aibu kwa muandaaji wa
mshindano hayo, Hashim Lundenga akidaiwa kupigwa changa la macho pindi
anapowapokea katika mchakato wa awali.
“Hii
ni aibu nyingine kwa Lundenga kwani haiwezekani mtu akaingia akasema
ana miaka kumi na nane halafu awe na elimu kama hiyo, anashindwaje
kulibaini hilo mapema?”
Alihoji
mdau mkubwa wa urembo nchini akikumbushia kisa cha Wema Isaac Sepetu,
Miss Tanzania 2006/07 ambaye naye alidanganya umri akasema ana miaka 18
wakati alikuwa na kumi na saba.
MSIKIE LUNDENGA SASA
Alipotafutwa Lundenga ili kuzungumzia suala hilo, alijibu kwa kifupi na kukata simu:
“I can’t answer that question (Siwezi kujibu swali hilo)…siwezi.”
SITTI ANASTAHILI KUWA NA UMRI GANI?
Ukiachilia
mbali muonekano, baadhi ya watu waliozungumza na mwandishi wa habari
hizi walisema kuwa ukifuata utaratibu wa mfumo wa elimu Bongo, Sitti
alipaswa angalau awe na umri wa miaka 23, hata kama madai ya kurushwa
madarasa ni sahihi.
Yaani
angeanza darasa la kwanza akiwa na miaka saba, angesoma shule ya msingi
kwa miaka saba, sekondari miaka minne, kidato cha tano na sita miaka
miwili na chuo miaka mitatu, jumla angekuwa na umri wa miaka 23 kwa sasa
ambayo ni pungufu ya miaka 25 iliyotajwa kwenye wasifu wake mtandaoni
huko nchini Marekani.
SITTI AMEFIKAJE HAPA?
Data
zinaonesha kwamba, baada ya kumaliza kidato cha sita, Sitti alihamia
jijini Dalas kwenye Jimbo la Texas, Marekani ambapo mbali na kusomea
elimu ya chuo kikuu nchini humo, amewahi kuigiza filamu inayojulikana
kwa jina la Lost In Abroad.
Hakuna maoni: