Watu 10 wanashikiliwa na
polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko
30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la
wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja
anayesadikiwa kuhusiana na watu hao waliokamatwa aliuawa na wananchi
wenye hasira baada ya kumjeruhi kwa panga askari polisi aliyekuwa
akipambana naye.
Akizungumza na waandishi
wa habari jana, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul alisema
tukio hilo lilitokea juzi (Aprili 14 mwaka huu) majira ya saa 3.30
usiku katika kitongoji cha Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani
Kilombero.
Kamanda Paul alimtaja
mtu aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo ambaye umri wake haujafahamika
ambaye ni mkazi Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha alisema siku ya
tukio polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao na
kwamba walitaarifiwa kuwa wanajihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu
na polisi waliamua kufatilia nyendo zao.
Akisimulia tukio hilo,
Kamanda Paul alisema: “Polisi walipata taarifa kuwa watu hao walitumia
usafiri wa bajaji mbili kwenda kusikojulikana na wakati wakiendelea na
zoezi la kufuatilia ndipo walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria
mmoja ambaye ni Mkwendo na kuisimamisha.”
Alisema kuwa bajaji hiyo
iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari
mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia
mtuhumiwa huyo alichomoa jambia alilokuwa nalo na kumkata askari huyo
eneo la shingoni.
Askari mwingine mwenye
namba E.9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma alifanikiwa kumpiga
risasi ya mguu mtuhumiwa huyo,ambapo alipoanguka chini wananchi wa eneo
hilo tayari walifika katika eneo hilo na kuanza kumshambulia marehemu
huyo kisha kumchoma moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi walipofika
katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti huo kuwatoa watu wote
waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa
mashaka,”Alisema kamanda Paul
Alisema polisi waliendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.
Kamanda huyo alitaja
vitu vilivyokutwa katika mabegi yaliyokuwa ndani ya msikiti huo ni
pamoja na milipuko 30, bendera nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu
yakisomeka ‘Mungu Mmoja’, majambia, bisibisi, vinyago vya kuziba uso
(masks), nguo za jeshi, misumeno ya chuma na spana.
Hakuna maoni: