Watanzania wanakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea
tetemeko la ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa wa
Kagera.
Tetemeko hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi,
uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya
Watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za
kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na
Kyerwa.
Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile,
nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi
zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya
kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya
yalisababisha uharibifu mbalimbali wa miundombinu ya barabara na majengo
ya watu na taasisi mbalimbali, ikiwemo shule na Hospitali.
Kufuatia maafa hayo, wananchi na taasisi mbalimbali, pamoja na nchi
marafiki, waliitikia wito wa kuwasaidia wahanga wa maafa na kukarabati
miundo mbinu iliyoharibika. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Fedha, Vyakula na
Vifaa mbalimbali vya Ujenzi vilikuwa vimepatikana kwa njia ya michango
mbalimbali.
Chama chetu kimeshtushwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwamba
Wananchi walioathirika wajitegemee wenyewe na kwamba misaada yote
iliyotolewa Ni ya Serikali na Taasisi zake tu.
Kauli hii ya Mkuu wa Mkoa haikubaliki kwani inadhalilisha waathirika na watu wote waliojitoa kuwasaidia waathirika hao.
Tunachukulia kauli hii kama tangazo la wizi wa uaminifu wa wananchi
waliochanga. Ni busara ya kawaida kuwa hatua ya kwanza katika
kushughulikia maafa ni kurudisha hali ya maisha ya watu katika hali ya
kawaida sambamba na ukarabati wa miundombinu. Aidha, suala la ujenzi wa
miundo mbinu ya taasisi za umma ni jukumu la msingi la serikali. Kwa
sababu hii:
• ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuu kujitenga na kufuta kauli ya mkuu
wa mkoa wa Kagera kwa sababu inaigombanisha serikali na wananchi
inaowaongoza.
• ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuelekeza ni misaada iliyopatikana
kwa michango ya wananchi, taasisi na nchi rafiki katika kusaidia
wananchi walioathirika kurudi katika maisha ya kawaida, ikiwemo
ukarabati na ujenzi wa nyumba za kuishi.
• ACT Wazalendo tunatoa wito kwa taasisi za kiraia nchini kuchukua
nafasi yake katika kuendelea kuikumbusha serikali wajibu wake wa msingi
wa kuboresha maisha ya watu.
Janeth Rithe
Katibu wa Taifa ACT Wazalendo, Kamati ya Maendeleo ya Jamii
13/11/2016, Dar Es salaam.
Hakuna maoni: