Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Fransisko
****
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Fransisko amemtunuku
tuzo ya heshima aliyekuwa mkuu wa Idara ya afya mstaafu wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Daktari Fredrick Kigadye kutokana na
mchango mkubwa alioutoa kwa kanisa Katoliki.
Mwadhama, Askofu Mkuu Polycarp Kardinali Pengo wa Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Fransisko alikabidhi tuzo hiyo kwa
daktari Kigadye jijini Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika
baraza la maaskofu. Baada ya kukabidhi tuzo hiyo Kardinali Pengo alisema
amejisikia furaha kwa tendo hilo kubwa katika kanisa lao hapa nchini la
daktari Kigadye kupewa tuzo hiyo.
“Daktari Kigadye ametusaidia sana katika masuala ya Pasada kwa hiyo nina
sababu ya ziada ya yale yaliyoongelewa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
tukio hili. Ni shukrani kubwa kwa Baba Mtakatifu Fransisko aliyeridhia
ombi la maaskofu kutoa hii hati pamoja na nishani.Hati ikitolewa na
Mwenyezi Mungu mambo mengine ni ziada,” alisema Pengo.
Naye daktari Kigadye alitoa shukrani zake kwa Mungu, Baba Mtakatifu
Fransisko na kwa maaskofu wote waliochangia jambo hilo kufanikiwa.
“Asante kwa Mwenyezi Mungu kwa uhai na majaliwa yote kwangu na wote
walioshiriki katika malezi yangu hadi kufikia siku ya leo kihistoria,”
alisema daktari Kigadye.
Kwa upande wake rais wa Maaskofu Katoliki Tanzania, Tarcisius
Ngalalekumtwa alimtaka daktari huyo asijisifu wala kujivuna kwa kuwa
jambo hilo lililofanyika ni kazi ya Mungu.
Tuzo hiyo ‘Bene Merenti’ maana yake ikiwa ni ‘kwa yule anayestahili’
ilipokelewa kwa furaha na katibu mkuu wa TEC, Padri Raymond Saba.
Hakuna maoni: